Kampuni za kokoto chalinze zalia na ushuru wa sh. 60,000 kwa lori-modest



NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
KAMPUNI ya uchimbaji
wa mawe na kusaga kokoto ya Gulf Aggregates(T), Lugoba imeitaka
halmashauri ya Chalinze na serikali kuangalia uwezekano wa
kuwashirikisha wawekezaji, kabla ya kufanya mabadiliko ama kuwapandishia
ushuru.
 
Aidha imeiomba halmashauri ya Chalinze, 
kuboresha miundombinu ya barabara ambayo imekuwa changamoto hususani
kipindi cha mvua huku barabara hiyo ikiwa tegemeo la magari ya kokoto
zaidi ya 500 yapitayo njia hiyo kila siku.
 
Akielezea changamoto
wanazokabiliana nazo wakati akizungumza na waandishi wa habari ,katika
maonyesho ya viwanda yanayoendelea mkoani Pwani, ofisa muajiri wa
kampuni hiyo,Agustine Modest alisema,kwasasa halmashauri hiyo
imepandisha ushuru kutoka sh.20,000 hadi 60,000 kwa lori kiasi ambacho
ni kikubwa kwao .
 
“Ushuru huu ni mkubwa
kwa mwekezaji lakini pia unatuumiza  kwani lazima gharama ya kuuza
itapanda, tunaomba ushuru upunguzwe hadi sh.30,000 aliomba.
 
Modest alisema,ushirikishwaji ni muhimu kwakuwa wamekuwa wakipandishiwa ushuru tofauti na faida wanayoipata hivyo kupata hasara.
 
Nae Ramadhani Siasa
ambaye ni meneja masoko wa Lake Gas alieleza, pia wanatarajia kuanza
uzalishaji wa mitungi ya gesi ambapo maandalizi yanatarajia kukamilika
mwezi desemba mwaka huu.
 
“Lake gas itakuwa ya
kwanza kwa uzalishaji wa mitungi hiyo hapa nchini ambapo awali mitungi
yote ilikuwa ikiagizwa kutoka nje ya nchi”alieleza Siasa.
 
Gulf Aggregates ni
kati ya makampuni yanayomilikiwa na Lake Group, makampuni mengine ni
Lake gas, Lake Oil, Lake Trans ,Lake petrolium,Lake steel na Lake
Cylinders.