Mbunge wa Arusha Mjini kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema, ametoa ofa ya magari 10
yatakayotumika kupigia matangazo ya hamasa kwa wananchi, kujitokeza
kushiriki vyema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza leo Oktoba 12, 2019 na EATV & EA Radio Digital, Lema
amesema kuwa ameamua kutoa ofa hiyo baada ya kuona magari yanayofanya
shughuli hiyo kuwa ni machache na kwamba yupo tayari yawekwe bendera za
Chama cha Mapinduzi (CCM).
”Nimewaomba niwape ofa ya magari matano mpaka kumi, watangazie wananchi
kwenda kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa,
wananchi hawajui na gari ni chache, kwahiyo kama wanahisi kutangazia
huko kunaweza kukasababisha wafuasi wengi wa CHADEMA, wakapata
‘awareness’ nimewaomba hayo magari yawekwe bendera za CCM lakini
niyalipie mimi” amesema Lema.
Kwa mujibu wa EATV, Hatua hii ya Lema kutoa ofa hiyo ni baada ya yeye
kupokea barua kutoka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya, iliyomzuia kufanya
mikutano yake ya hadhara jimboni kwake, ambapo hapo siku ya jana Oktoba
11, 2019, aliruhusiwa kuendelea na mikutano yake kama kawaida.