Tanesco yakusanya bilioni 46 kwa wiki

Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa sasa linakusanya shilingi bilioni 46
kwa wiki hali inayofanya Shirika hilo kuendelea kujitegemea baada ya
kuacha kupokea ruzuku kutoka serikalini ili kujiendesha.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani tarehe 18
Oktoba, 2019 wakati wa kikao chake na wafanyakazi wa TANESCO wa Kanda ya
kaskazini kilichofanyika jijini Tanga na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa
Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Nishati, Raphael Nombo na
viongozi kutoka TANESCO Makao Makuu.
” Niwapongeze TANESCO kwa kuendelea kujiendesha kwani hampokei tena
ruzuku kutoka Serikalini na sasa mnakusanya shilingi Bilioni 46 kwa wiki
tofauti na miaka miaka miwili iliyopita mlipokuwa mkikusanya bilioni
Sita hadi Tisa kwa wiki, mnao uwezo, endeleeni.”alisema Dkt Kalemani
Kuhusu mkakati wa kuongeza mapato ya Shirika alisema kuwa, kunzia mwaka
huu wa fedha, Kila Ofisi ya Mkoa ya TANESCO itapewa malengo ya makusanyo
na atakayefikia malengo hayo atapewa motisha, ila atakayeshindwa
atachukuliwa hatua.
Kuhusu ongezeko la wateja waliounganishwa na umeme, Dkt Kalemani
ameliagiza Shirika hilo kufanya kazi kama makampuni ya simu kwa kufuata
wateja kule waliko ili idadi ya wateja hao iongezeke na hivyo mapato ya
Shirika kuongezeka.
Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani alisema kuwa, kuanzia sasa miradi
yote ya TANESCO inayotekelezwa kwa fedha za ndani itasimamiwa na
wataalam wa ndani ya nchi ukiwemo mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa
Julius Nyerere (MW 2115).
” Niwapongeze TANESCO kwa kusimamia mradi huu mkubwa wa Julius Nyerere,
zamani tulikuwa tukisimamiwa lakini sasa tunawasimamia wakandarasi na
hii inaokoa fedha za Serikali ambazo zingetumika kutafuta wasimamizi wa
miradi kutoka nje ya nchi kuja kusimamia miradi yetu.” alisema Waziri wa
Nishati
Kuhusu suala la umeme vijijini, Dkt. Kalemani alisema kuwa bei ya umeme
vijijini ni shilingi 27,000 bila kujali umbali aliopo mteja hivyo kila
mtumishi ahakikishe hilo linatekelezeka.
Aidha, aliagiza wataalam wa TANESCO kuacha mara moja lugha  lugha ya
“hakuna vifaa” ambayo mara kadhaa imekuwa ikitumika wakati wateja
wanapotaka kuunganishiwa umeme na kueleza kuwa vifaa vya umeme kama vile
nguzo, mita, transfoma na nyaya vinazalishwa ndani ya nchi na
kupatikana kwa urahisi hivyo lugha za visingizio zisiwepo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Raphael Nombo
alizungumza na wafanyakazi hao kuhusu masuala ya muundo wa TANESCO,
mikataba  ya wafanyakazi na suala la mishahara.
TANESCO, Kanda ya Kaskazini inajumuisha mikoa minne ambayo ni Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara.