Waziri mkuu majaliwa aagiza waliokula fedha za maji wakamatwe

WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kukamatwa na kuwekwa ndani viongozi wa
kamati ya watumiaji maji wa mradi wa maji wa Matunguru uliopo katika
Kijiji cha Tungamalenga wilayani Iringa kwa tuhuma za ubadhilifu wa sh.
milioni saba.





Ametoa
agizo hilo jana jioni (Jumamosi, Septemba 28, 2019) baada ya kupokea
malalamiko kutoka kwa wananchi wakati akihutubia  mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Kijiji cha Idodi wilayani Iringa.

Waziri
Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela afuatilie
suala hilo kwa kuwa kamati nyingi za watumiaji maji zimekuwa na tuhuma
za matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa kutoka kwa wananchi jambo
ambalo si sahihi.

Alisema
ifikapo saa 4.00 asubuhi ya leo watuhumiwa wote wanaohusika na
ubadhilifu huo wawe wameshakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola
kwa ajili ya kwenda kujibu tuhuma zinazowakabili.

Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema kwamba Serikali itajenga kwa
kiwango cha lami barabara ya kutoka Iringa hadi Ruaha yenye urefu wa
kilomita 104 ili kuboresha huduma za usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo
na kuinua uchumi.

Waziri
Mkuu aliyasema hayo baada ya kupokea malalamiko ya ubovu wa barabara
hiyo kutoka kwa mbunge wa jimbo la Ismani, William Lukuvu ambaye pia ni
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mbunge
huyo alisema licha ya Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo ikiwemo ya maji, afya na
umeme, lakini wanakabiliwa na tatizo la ubovu wa barabara ambapo aliomba
Serikali iwasaidie.

Baada
ya Waziri Mkuu kusema kuwa Serikali itahakikisha barabara hiyo
itajengwa kwa kiwango cha lami wananchi walifurahi na kuishukuru
Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa
kuwajali wananchi wake.

Awali,
Waziri Mkuu alikagua na kuzindua majengo matano ya kituo cha afya Idodi
ambayo yamegharimu sh. milioni 400. Pia Serikali iliongeza sh. milioni
300 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Waziri Mkuu alisema ameridhishwa
na ujenzi wa mradi huo.

Kwa
upande waobaadhi ya wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Mama na Mtoto
ambao walikuwa wajifungua kwa njia ya upasuaji waliishukuru Serikali kwa
kuboresha na kusogeza huduma za afya karibu na makazi ya wananchi.

Mmoja
wa wagonjwa hao, Agusta Nyagawa alisema awali walikuwa wanalazimika
kwenda hadi Iringa mjini kwa ajili ya kufuata huduma za afya lakini kwa
sasa huduma hizo zikiwemo za kujifungua pamoja na vipimo wanazipata
kituoni hapo.

Naye,
Chipe Ngugi alisema anaishukuru Serikali kwa kuwa huduma za afya
zimeboreshwa katika hospitali yao ya kata, hivyo hawatalazimika tena
kusafiri umbali mrefu hadi Iringa kwa ajili ya kufuata huduma za afya
zikiwemo za  upasuaji.

Alisema
yeye alijifungua kwa njia ya upasuaji na anawashuwashukuru madaktari na
wauguzi  kituoni hapo kwa huduma nzuri ambazo zimeokoa  Maisha yake na
mtoto. Aliiomba Serikali iendelee kuboresha huduma kwa kuwa wapo mbali
na mjini.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,