Kituo cha uchenjuaji dhahabu jema afrika chapewa onyo la mwisho

Waziri
wa Madini Doto Biteko ametoa Onyo la Mwisho la Kukifungia Kituo cha
Uchenjuaji Dhahabu cha Jema Afrika kilichopo Wilayani Kahama.


Hatua
hiyo inafuatia kubainika kwa jaribio la wizi wa dhahabu uliofanywa na
baadhi ya wafanyakazi wa  kituo hicho kutaka kuiba dhahabu ya mteja.



Akizungumzia
tukio hilo, Waziri Biteko amewataka wamiliki wa kituo hicho kuandika
barua ya kuweka makubaliano na Serikali ya kutojirudia tena kwa vitendo 
vya wizi kituoni hapo.

‘’Ni
jicho la huruma tu  tukiwapeleka mahakamani mali zenu zitataifishwa.
Tunajua mmewekeza mitaji yenu na mna mikopo.  Nilishamwambia mmiliki
kuwa kituo  chako kina rekodi ya wizi. Rais anawapenda, anawapigania ili
watanzania wamiliki uchumi wa madini lakini mnamuangusha kwa kutofuata
taratibu,’’ amesisitiza Waziri Biteko.

Amewatahadharisha
wamiliki wa vituo vya uchenjuaji nchini kuhusu wizi wote wa dhahabu 
unaofanyika na kuwasisitiza kwamba, unafahamika na kuwataka  wote
wanaojihusisha na vitendo hivyo  kujiepusha  na  kwa wale wasiotaka
kufanya kazi zao kwa  uaminifu watafute biashara nyingine.

Mbali
na kutembelea kituo hicho,  pia, Waziri Biteko  na ujumbe wake 
wametembelea Kituo Kidogo cha  Ununuzi   wa dhahabu kilichopo katika
eneo la Wachimbaji wadogo wa Mwime  ambapo amewapongeza kwa kufuata
taratibu na Sheria na kuwataka kufanya kazi zao kwa amani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga  Zainab Taleck amesema  Mkoa huo unahitaji wawekezaji lakini walio waaminifu.

Ameongeza
kuwa, wizi na udanganyifu katika kiwand cha uchenjuaji Jema Afrika
ulibainiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama na kutumia fursa hiyo
kuwatahadharisha wote wasiofuata taratibu kuwa serikali inawaona na
itawafikia.

Katika
ziara hiyo, Waziri Biteko pia ameongozana na Naibu Waziri wa Madini
Stanslaus Nyongo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga,
Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa na Watalaam kutoka Tume ya
Madini.

Aidha,
ziara hiyo imefanywa wakati ambapo wizara na wadau wengine wa madini
wanashiriki Maonesho ya Pili ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya
Madini Mkoani Geita yanayotarajiwa kuhitimishwa Septemba 29, 2019.

Ziara hiyo imefanyika Septemba 28, 2019