Mjane alazimika kuishi kwenye kibanda porini kukwepa manyanyaso ya watoto

Mjane Mariam Mnyang’au (55)mkazi wa kijiji cha Mahenge wilaya ya Kilolo
mkoani Iringa akiwa katika makazi yake porini baada ya kudai kunyanyaswa
na watoto wake baada ya mume wake kufariki (PICHA NA FRANCIS GODWIN

Na Francis Godwin Iringa 

Mwanamke mjane
mkazi wa kijiji cha Mahenge wilaya ya Kilolo mkoa wa Iringa Mariam
Laurent Mnyang’au (55) amejikuta katika mateso makubwa baada ya
manyanyaso anayopata kutoka kwa watoto wake hivyo kulazimika kukimbia
nyumba na kwenda kuishi porini mwenyewe kukwepa mateso.

Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi aliyemtembelea eneo la pori analoishi
kwenye kibanda ambacho kimejengwa kwa miti na kuezekwa nyasi eneo  moja
pekee ambalo  ametandika mkeka wa kulalia na robo tatu ya kibanda hicho
ikiwa wazi. 

Mwanamke huyo alisema kuwa mateso
hayo yamekuja baada ya mume wake kufariki  na watoto hao  kuanza kumtesa
kwa lugha cha matusi na hata kutishia kumpiga wakitaka kuachiwa mali
mbali mbali alizoziacha  marehemu mume wake. 

“Tatizo
mume wangu alikuwa  ametuoa wanawake wawili bibi mkubwa yupo na mimi ni
bibi mdogo sasa watoto wake ni magaidi sana wamekuwa wakishirikiana nae
kuninyanyasa pale nyumbani kweli nilishindwa uvumilivu nikaamua kuja
kuishi hapo “alisema 

Alisema zaidi ya miaka 25
amedumu kwenye ndoa na mume hyo ila toka afariki  amekuwa akiishi kwa
mateso toka mumewe alipofariki dunia na kuwa pamoja na mali nyingine
marehemu alikuwa na nyumba ila mali zote aliziacha na kuondoka na nguo
zake pekee kwenda porini hapo kuanza maisha mapya. 

Aidha
alisema tatizo  jingine la mateso na kukosa kudai mali ni kitendo cha
kutoachwa wosia wowote na kama kungekuwa na wosia basi amgeweza kudai
mali zake .

Hata hivyo alisema mwanga wa kuanza
kupambana kutafuta ardhi ya kumiliki mwenyewe aliupata baada ya elimu
iliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la ISICO chini ya mratibu
wake Raphael Mtitu hivyo kutokana na elimu ya haki ya wanawake na watoto
wa kike kumilikishwa mali kijiji kilikwenda mpimia eneo hilo alilojenga
na kwa nguvu yake kajenga kibanda hicho.

“Ninatamani
kuwa na nyumba ya kisasa kama wasamaria wema watajitokeza kunisaidia
ila kwa sasa uwezo wangu umeishia hapa na sijui kipindi cha mvua hali
itakuwaje maana sijaweza funika sehemu yote ya kibanda na kama unavyoona
kibanda hakina hata mlango na huku kwetu mara moja moja tembo huwa
wanakatisha ila namwachia ulinzi Mungu kwani kwa sasa ana miezi miwili
eneo hilo.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha
Mahenge Said Mhina alisema kijiji kimekuwa na utaratibu wa
kuwamilikisha Ardhi wanawake na kuwa mwanamke huyo baada ya kufika
ofisini kuomba ardhi alipewa eneo hilo ambalo limetengwa kwa ajili ya
makazi .

Kuwa wanawake wanaoteseka katika ndoa kwa kutopewa Ardhi kijiji kimeanza kuwapa maeneo ya kujenga na kulima. 

Mratibu
wa ICISO Raphael Mtitu alisema toka shirika lake limeanza kutoka elimu
vijiji wanawake na watoto wa kike sasa wameanza kupewa haki sawa katika
umiliki wa mali na kupongeza kijiji cha Mahenge kwa kutoa Ardhi kwa
mjane huyo huyo.

Kwa mawasiliano na mwanamke huyo wasiliana na mwandishi wetu Francis Godwin 0754026299