Serikali yafuta mapori tengefu 12 na hifadhi saba


Serikali
imeridhia kufuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94
ambayo yamepoteza sifa na imeamua yagawiwe kwa wananchi kwa ajili ya
shughuli za makazi, kilimo na mifugo.

Uamuzi huo umefikiwa leo (Jumatatu, Septemba 23, 2019) kwenye kikao cha
Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania; Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa mara baada ya kikao hicho, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amesema Mawaziri wa kisekta wakiongozwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi walichambua na kuandaa taarifa
ya mapendekezo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi nchini
iliyowasilishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha leo.
“Mawaziri walichambua na kubaini kuwa vijiji vyenye migogoro ni 975 na
siyo 366 kama ilivyotangazwa awali, Baraza limeamua kwamba vijiji 920
vitabaki ndani ya hifadhi, mipaka irejewe upya, vipatiwe vyeti vya ardhi
vya kijiji pamoja na kupangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi,”
amesema na kuongeza kuwa orodha ya vijiji hivyo itatangazwa baadaye.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeridhia Misitu ya Hifadhi saba yenye
ukubwa wa ekari 46,715 iliyopoteza sifa itolewe kwa wananchi kwa ajili
ya shughuli za makazi, kilimo na mifugo ili kuwaondolea kero za uhaba wa
ardhi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeridhia kumega hifadhi za
misitu 14 kwa ajili ya kilimo na mifugo na kufuta mashamba 16
yasiyoendelezwa ili yapangiwe matumizi ya kilimo na mifugo.
“Vijiji 55 vilivyobaki vinaendelea kufanyiwa tathmini ya kina maeneo
yaliyobaki ndani ya hifadhi na kuwasilisha mapendekezo yake kwa ajili ya
uamuzi. Uchambuzi na taarifa itatolewa,” amesema na kuongeza kuwa
orodha ya maeneo ya vijiji, mapori ya wanyama, misitu na mashamba
yaliyofutwa itatangwa baadaye.
Pia amesema Baraza limeamua ardhi ya mita 500 zilizotengwa kama buffer
zone (eneo kinga) kwenye maeneo ya vijiji vinavyopakana na hifadhi za
wanyama ziachiwe vijiji husika na wananchi wasiondolewe kwenye maeneo
hayo.
Ameyataja maamuzi mengine yaliyofikiwa kwenye kikao hicho kuwa ni Ofisi
ya Makamu wa Rais imetakiwa ikamilishe mwongozo utakaobainisha matumizi
ya ardhi ndani ya hifadhi ya mita 60 za mito, vyanzo vya maji, maziwa na
bahari.
Maamuzi mengine ni kuzitaka Wizara na taasisi zote za Serikali zilinde
maeneo yao kwa kuweka alama za kudumu zinazoonekana; na kwamba wananchi
hawaruhusiwi kuvamia maeneo mapya na hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya uvamizi wowote kuanzia leo.
Januari, mwaka huu, Rais Magufuli alitoa maagizo kwa Mawaziri nane  wa
sekta zinazohusika na matumizi ya ardhi wachambue na kuandaa taarifa ya
mapendekezo ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi nchini.
Maagizo hayo yalikuwa ni pamoja na: Kutoviondoa vijiji na vitongoji 366
vilivyomo ndani ya hifadhi; Kubainisha maeneo ya hifadhi ambayo
yamepoteza sifa ili yaweze kugawiwa kwa wananchi kwa shughuli za ufugaji
na kilimo na kuhakiki na kurekebisha mipaka baina ya hifadhi za misitu,
wanyama na makazi.
Mengine ni kumega baadhi ya hifadhi za Taifa, mapori tengefu na misitu,
kuwagawia wafugaji na wakulima; Kufanya mapitio ya sheria mbalimbali
zinazohusiana na matumizi ya ardhi; Kupitia upya Sheria ya Vyanzo vya
Maji inayozungumzia uhifadhi ndani ya mita 60; Kuwasilisha mapendekezo
ya kufutwa mashamba yasiyoendelezwa na kugawa kwa wananchi kwa ajili ya
uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo na kuendelea kulinda na
kuhifadhi maeneo ya hifadhi za misitu, wanyamapori na vyanzo vya maji.