Shivyawata waiomba serikali kutilia mkazo ukatili wa kijinsia kwa watu wenye ulemvu

Kaimu
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Watoto kutoka Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwajuma Magwiza (Kushoto)
akielezea namna Wizara inavyoshugulikia masuala ya ukatili dhidi ya
watoto wakiwemo wenye ulemavu katika kikao kati ya Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Waziri Mkuu
Kitengo kinachoshughulikia watu wenye ulemavu.
SHIRIKISHO la Vyama vya Walemavu (SHIVYAWATA) limeiomba
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jmaii, Jinsia, Wazee na Watoto kuongeza
nguvu katika kutoa elimu kwa umma juu ya kupambana na manyanyaso na
vitendo ya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu nchini.


Ombi hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Mwenyekiti wa SHIVYAWATA
Taifa Ummy Hamisi Nderiananga wakati wa kikao kati ya Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Waziri Mkuu
Kitengo kinachoshughulikia watu wenye ulemavu.


Ummy ameongeza kuwa kama Wizara ilivyoweka nguvu kwenye masuala ya
jinsia hasa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto basi pia
waongeze nguvu katika kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya walemavu
katika jamii.


“Vitendo vya ukatili dhidi ya walemavu wawe watoto au wanawake hata
wanaume pia vinatendeka katika familia zatu ila havipigiwi kelele za
kutosha” alisema Ummy.


Ummy amesisitiza Wizara kupitia Mpango Mkakati wa Taifa wa kupambana
na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ili uweze kuwezesha kuingiza
masuala ya watu wenye ulemavu ili kuondokana na vitendo vya kikatili
vinavyowapata watu wenye ulemavu nchini.


Akifafanua kuhusu Wizara kutilia Mkazo suala la Ukatili dhidi ya watu
wenye ulemavu Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Watoto kutoka
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwajuma
Magwiza amesema kuwa Wizara inalenga kupambana na vitendo vya ukatili
dhidi ya makundi yote ikiwemo kundi la watu wenye ulemavu nchini.


Mwajuma ameongeza kuwa Wizara imejikita katika Kampeni mbalimbali za
kupambana na vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto likiwemo
kundi la watu wenye elemavu kwa kutoa elimu kwa jamii ya kupambana na
vitendo hivyo.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Patrick
Golwike amesema kuwa kikao hicho kimeisaidia Wizara kupata namna bora ya
kuyafikia makundi ya watu wenye ulemavu kabla ya kuandaa miongozi na
Mikakati mbalimbali ya Wizara ili katika utekelezaji wake isiache kundi
la watu wenye ulemavu na makundi mengine maalum.


Golwike ameongeza kuwa Wizara itashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu
Kitengo cha watu wenye ulemavu katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira
wezeshi kwa watu wenye ulemavu katika kapata fursa sawa kama makundi
mengine katika jamii hasa katika utoaji wa mikopo na elimu ya
ujasirimali.


Naye Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha watu wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya
Waziri Mkuu Philbert Kawemama amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu
inafuatilia utekelezaji wa Sheria namba 9 ya mwaka 2010 na Kanuni zake
ili kuhakikisha kila Wizara na Taasisi zake zinazingatia masuala ya watu
wenye ulemavu katika kuhakikisha wanapata mazingira stahiki katika
utekelezaji wa majukumu yao.


Ameongeza kuwa pia Ofisi ya Waziri Mkuu inafuatilia uwezeshwaji wa
kundi la watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha wanapata fursa sawa za
kimaendeleo na kusaidia kundi hilo kuondokana na vitendo vya unyanyapaa
na vitendo vya kikatili dhidi yao.


Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la ADD International Isack
Idama amesema kuwa Wizara ina dhamana kubwa kwa maendeleo ya watoto na
wao kama wadau wa masuala ya watu wenye ulemavu hasa watoto wangependa
kuona kwa jinsi gani masuala ya watoto wenye ulemavu yanashughulikiwa.


Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo kinachoshughulikia watu wenye ulemavu
kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania
wanatembela Wizara na Taasisi za Serikali katika kufuatilia na kuona kwa
jinsi gani masuala ya watu wenye ulemavu yatekelezwa.