Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Asasi za Kijamii, ikiwemo
HakiElimu, katika kuweka mkazo kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike
kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa jumla.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa uzinduzi
wa ripoti ya utafiti ya HakiElimu kuhusu changamoto za Elimu ya mtoto
wa Kike.
Dkt. Akwilapo amesema nia ya Serikali ni kushirikiana na wadau wa elimu
ili kuona kuwa vikwazo vyote dhidi ya elimu kwa mtoto wa kike vinapatiwa
suluhisho sahihi.
“Ili kufanya maamuzi sahihi, Wizara ninayoiongoza hutumia uthibitisho
unaotokana na tafiti mbalimbali zinazofanywa na Wizara yenyewe na wadau
wengine wa elimu. Sisi kama watunga sera hatuwezi kufanya kazi kwa
ufanisi bila ya kutumia matokeo ya utafiti,” Alisema Dkt. Akwilapo.
Dkt Akwilapo ameipongeza Taasisi ya HakiElimu kwa kuwa mstari wa mbele
katika kufanya tafiti mbalimbali ambazo zinatoa mchango mkubwa katika
sekta ya elimu.
“Ripoti ya utafiti ninayoizindua leo ni mfano hai wa kile ninachokisema
kuhusu mchango wa Sekta binafsi kwani inahusu changamoto zinazosababisha
wasichana kushindwa kuendelea na masomo na kuvuka katika hatua
nyingine. Utafiti huu unaendana na lengo la Serikali la kuhakikisha kuwa
wasichana wanaoandikishwa katika Elimumsingi wanamaliza safari yao ya
elimu kwa mafanikio makubwa,” aliongeza Dkt. Akwilapo.
Akizungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha mtoto
wa kike anapata elimu Dkt. Akwilapo amesema Serikali imekuja na Sera ya
Elimu bila malipo katika ngazi ya Elimumsingi ambayo imewezesha
wasichana wengi kuandikishwa katika shule ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa
mabweni ambayo yamesaidia kuwaweka wasichana karibu na shule na kuepuka
vishawishi vya barabarani wakati wa kwenda na kurudi shule.
Jitihada nyingine ni kutunga sheria ambayo inawabana watu wanaotaka kuoa
watoto wa shule au kushirikiana nao kimapenzi, na hivyo kuwaharibia
masomo kwa kuwapa ujauzito pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu
umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
Naye Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu, Dkt. John Kalaghe amesema azma ya
kufanya utafiti huu imechagizwa na kampeni ya Elimu ya mtoto wa kike
ambayo HakiElimu inaifanya. Amesema kampeni hiyo ni sehemu ya
utekelezaji wa mpango mkakati wa mwaka 2017 hadi 2021 ambao wamejiwekea
na umejikita katika kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali
kuhakikisha kwamba watoto wa kitanzania wakiwemo watoto wa kike wanapata
elimu bora itakayowawezesha kukabili changamoto katika maisha yao na
kusaidia ujenzi wa Taifa letu.
“HakiElimu tunatilia mkazo katika kuhamasisha utolewaji wa elimu
jumuishi yenye ubora na usawa pamoja na elimu kwa watoto wa kike ikiwa
ni pamoja na kupunguza au kuondoa kabisa unyanyasaji wa watoto shuleni
na nje ya mipaka ya shule,” Alisema Dkt. Kalaghe.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
20/09/2019.