Wanafunzi wanaotuhumiwa kumuuwa mwenzao waruhusiwa kujisomea wakiwa magereza kagera

Na Silvia Mchuruza:
Kagera:
Kufuatia kesi ya
mauaji ya mwanafunzi Mudy Muswadiku wa shule ya sekondari  Katoro
Islamic Seminary  ya mkoani Kagera wanafunzi wanaotuhumiwa katika mauaji
hayo wameruhusiwa kuendelea kujisomea wakiwa gerezani ili kujiandaa na
mtihani wa kidato cha nne unaotarajiwa kuanza Novemba 4, mwaka huu
nchini.

Ruhusa hiyo imetolewa
na mahakama baada ya Majaliwa Abdu (mwalimu) ambaye ni miongoni mwa
watuhumiwa katika shitaka hilo kuwasilisha maombi matatu kwa mahakama
leo (Jana), kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya pili katika Mahakama ya
Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.

Majaliwa aliiomba
mahakama hati ya mashtaka pia aliomba upelelezi wa kesi hiyo uwahishwe
ili kama wanafunzi hawatakuwa na hatia waweze kurudi shuleni kuendelea
na masomo na kujiandaa na mitihani inayowakabili baadhi yao.

Ombi la tatu,
Majaliwa aliiomba mahakama kuwaruhusu wanafunzi wa kidato cha nne
wanaotuhumiwa katika kesi hiyo kuruhusiwa kuwa na madaftari gerezani ili
waweze kuendelea kujisomea na kujiandaa na mitihani inayotarajiwa
kuanza Novemba 4, mwaka huu.

Kufuatia maombi hayo,
Wakili wa Serikali mkoani Kagera, Haruna Shomari alisema watuhumiwa hao
watapatiwa hati hiyo ya mashtaka leo (Jana) na pia vitu kama madaftari,
vitabu na kalamu wanaruhusiwa kuwa navyo gerezani.

Aliwataka wanafunzi
hao wawasiliane na Mamlaka ya Magereza ili waweze kuletewa madaftari,
vitabu na kalamu ili waendelee kujisomea wakiwa gerezani ili kujiandaa
na mitihani hiyo.

Katika kesi hiyo pia
idadi ya watuhumiwa wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya mwanafunzi huyo
aliyekuwa anasoma kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Katoro
Islamic ya mkoani Kagera, imeongezeka baada ya wanafunzi wengine wawili
kuongezwa katika shitaka hilo. 

Wanafunzi waliongezwa
ni Sharifu Amri (19) na Fahadi Abdulazizi Kamaga (20) na kusababisha
idadi ya watuhumiwa kufikia wanafunzi sita, mwalimu mmoja na mlinzi
mmoja wa shule hiyo.

Kesi hiyo ya mauji
namba 18/2019 inayosikilizwa na Hakimu Frola Kaijage, imetajwa kwa mara
ya pili leo (Jana) katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera.

Watuhumiwa wengine
wanaokabiliwa na kesi hiyo ni wanafunzi Husama Ramadhan (17), Sharifu
Huled (19), Abdalah Juma (19) na Hussein Mussa (20), Majaliwa Abud (35)
mwalimu na Badru Issa Tibagililwa (27) mlinzi.

Kesi hiyo
imehairishwa hadi Septemba 30 mwaka huu ambapo pia itatajwa tena kwani
mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza shitaka hilo.

Wakili Shomari
amesema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kuwa wanafunzi
walioongezwa, nao wamebainika walishiriki kumpiga Mudy (marehemu).

“Katika upelelezi
tunaoendelea kuifanya tulibaini kuwa pia wanafunzi hao wawili
walioongezwa nao walishiriki kumpiga marehemu (Mudy) wakati huo huo bado
upelelezi unaendelea,” alisema Shomari.

Mauji hayo yalitokea
Aprili 14 mwaka katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic iliyoko
katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera.

Watuhumiwa wamerudishwa rumande hadi siku kesi itakapotajwa tena.