Vyama vya siasa vyaonywa kupeleka majina ya wagombea wasio na sifa uchaguzi serikali za mitaa


Na Ashura Jumapili, Bukoba
Serikali mkoani Kagera itakichukulia hatua kali  chama chochote cha
siasa kitakachopeleka jina la mgombea asiyekuwa na sifa kwa mujibu wa
sheria za uchaguzi katika uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa
unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 ,Novemba mwaka huu.



Onyo hilo limetolewa leo Septemba 12,2019 na Katibu Tawala Mkoa wa
Kagera Prof. Faustine Kamuzora wakati wa kuapishwa kwa wateule wa
usimamizi nane wa uchaguzi kutoka halmashauri zote za mkoa huo. 






Alisema mkoa umeshatoa maelekezo kuwa majina ya wagombea yatakayopelekwa
kwa wasimamizi wa uchaguzi lazima awe raia wa Tanzania kwa mujibu wa
sheria na kanuni za uchaguzi.






Alisema wananchi wanayo haki ya kupinga mgombea ambaye uraia wake una mashaka .






“Chama kitakacholeta mgombea mwenye uraia unaotiliwa mashaka kitapoteza
nafasi kwa sababu kanuni zinaonyesha sifa za mgombea ya kwanza no
lazima awe raia wa Tanzania”, alisema Prof.Kamuzora. 






Alisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika na hivyo
kuwataka wananchi wawe walinzi dhidi ya watu wanaojipenyeza kugombea
wasiokuwa na sifa hasa Wilaya za Ngara,Kyerwa na Missenyi.






Aliwaomba wateule hao wa usimamizi wa uchaguzi kusoma zaidi maandiko ili waweze kuelewa majukumu yao katika uchaguzi huo.






“Nimefarijika sana kuona nusu ya wateule ni wanafunzi wangu.Hakikisheni
hamcheleweshi wala kuwa sehemu ya kusababisha matatizo”,alisema
Kamuzora.






Wateule hao wameapishwa na hakimu mkazi mahakama ya wilaya ya Bukoba Frola Kaijage.






Kaijage alisema wakienda kinyume sheria inachukua hatua ya kijinai na taratibu za kinidhamu.






Waliopishwa ni Costantino Msemwa kutoka Biharamulo mkuu wa idara ya
Mipango takwimu na ufuataliaji,Babylus Mashauri kutoka halmashauri ya
Bukoba mkuu wa idara ya Kilimo ,umwagiliaji na ushirika,Bukoba manispaa
Richard Mihayo mkuu wa idara ya Mipango takwimu na ufuatiliaji.