Wanufaika wa tasaf wilayani ngara washiriki kikamilifu katika miradi ya kutoa ajira ya muda

Na Mwandishi Wetu, APC BLOG, KAGERA

Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF wilayani Ngara mkoani Kagera, wamepongezwa kwa kushiriki katika miradi ya kutoa Ajira ya Muda (PWP) ambayo imewaongezea ujuzi wa kuanzisha miradi yao binafsi ili  kujiongezea kipato na kuboresha maisha yao.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) alipokuwa akizungumza na wananchi na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika vijiji vya Mayenzi na Murugina akiwa katika  ziara ya kikazi kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuzungumza na Watumishi wa Umma wilayani humo kuhimiza uwajibikaji.

Dkt. Mwanjelwa amesema, mafanikio waliyoanza kupata wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ni kielelezo kizuri cha manufaa ya kuwahusisha Walengwa hao kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia nguvu kazi yao jambo ambalo amesema limepewa mkazo hata katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2015-2020.


Akiwa katika kijiji cha Mayenzi wilayani Ngara, Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa amejionea Shamba Darasa la miti aina ya Mikaratusi lenye ukumbwa wa ekari 14 ambalo wanufaika wa TASAF wamepanda miti ipatayo elfu Saba kwa kutumia utaratibu wa Ajira ya Muda.

Naibu Waziri huyo ameeleza kuridhishwa na jitihada hizo na kuagiza Wataalamu wa sekta ya misitu na nyinginezo nchini kuwa karibu na Walengwa wa TASAF wanaotekeleza miradi hiyo kuwa karibu ili kuwapatia elimu sahihi ya kutekeleza miradi hiyo ili iwe na tija.

Aidha, Dkt Mwanjelwa akiwa katika kijiji cha Murugina amejionea barabara iliyojengwa na Walengwa wa TASAF kwa kupitia utaratibu wa Miradi ya Ajira ya Muda, barabara ambayo imewaondolea kero ya usafiri kijijini hapo na kusaidia uendeshaji wa shughuli za kiuchumi ikiwemo kusafirisha mazao yao kwenda katika masoko.

Katika hatua nyingine, Dkt Mwanjelwa amewataka wataalamu na viongozi katika maeneo ambako Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kote unatekelezwa, kuonyesha mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Mpango huo hususani katika Nyanja za elimu, afya, maji, kilimo na mifugo kwenye maeneo yao ili uwe endelevu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akicheza ngoma na wananchi na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini alipowasili katika Kijiji
cha Murugina wilayani Ngara kukagua utekelezaji wa miradi ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akipokelewa kwa burudani ya ngoma na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini alipowasili katika Kijiji cha Murugina wilayani Ngara kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mhe. Alex Gashaza.


Dkt. Mwanjelwa anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Kagera ya kukagua miradi ya TASAF na kuzungumza na watumishi wa umma ambapo tayari ameshatembelea Manispaa na Halmashauri za Wilaya ya Bukoba, Biharamulo, Muleba na Ngara.