Na Claud Gwandu, Arusha.
JUMUIYA ya Vijana kwa ajili ya Ardhi barani Afrika (YILAA) inajiandaa kufanya utafiti wa kina wa kujua ushiriki wa vijana katika masuala ya Utawala wa Ardhi barani humo ili kuwa na majibu ya uhakika ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Tayari,Jumuiya hiyo imeandaa mpango kazi wa kufanya utafiti huo katika nchi za Benin, Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Tanzania.
Akizungumza baada ya ufunguzi wa Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Vijana na Utawala wa Ardhi barani Afrika(CIGOFA 4) jijini hapa leo,Ofisa Mtendaji Mkuu wa YILAA,Innocent Antoine Houedji amesema changamoto zinazowakabili vijana zinahitaji majawabu ya kisayansi.
Amesema,kwa kushirikiana na wadau na washirika mbalimbali,tayari wamefanikiwa kupata mafungu ya kufanya utafiti huo muhimu katika nchi za Benin na Senegal zilizopo Afrika Magharibi.
“Kama tunavyopanga utafiti wa kisayansi utaanza pengine mapema mwakani,na llengo ni kuwa na takwimu sahihi za kuelewa changamoto zinazowakabili vijana katika Utawala wa Ardhi barani Afrika.
” Tutashirikisha wadau wote muhimu ikiwa ni pamoja na serikali katika kufanikisha jukumu hilo na kisha tutaweka mikakati ya pamoja kukabiliana na changamoto hizo,”anasema.
Kuhusu Tanzania na DRC, Houedji anasema utafiti katika nchi hizo utafanyika baadaye na kwamba Mipango ya kutafuta wadau na washirika watakaofadhili utafiti huo inaendelea.
Vijana wengi kutoka Afrika Magharibi, katika miaka ya karibuni wamekuwa wakipoteza maisha wakijaribu kuzamia Ulaya kwa matumaini ya kupata maisha mazuri.
Wengi wamekuwa wakitumia vyombo hafifu vya kusafiri kupitia Bahari ya Mediterania,na wamekuwa wakizama baharini kutokana na uhafifu wa vyombo vya usafiri wanavyotumia.
Kwa upande wake.Mkurugenzi Mkazi wa YILAA tawi la Tanzania,Augustine Nyakatoma,anasema vijana wa Tanzania wanahitaji kuelimishwa na kuhamasishwa jjuu ya umuhimu wa kumiliki na matumizi sahihi ya Ardhi.
“Changamoto ni nyingi na tunahitaji majibu ya kisayansi kukabiliana nazo lakini wakati tunasubiri utafiti, tunawaelimisha kwa kutumia njia mbalimbali.
“Mikutano kama hii ambako mada mbalimbali zinawasilishwa ni njia mojawapo itakayosaidia kuongeza uelewa wa vijana katika Utawala wa Ardhi,” amefafanua.
Akitoa mfano, Nyakatoma anaitaja Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 nchini haijaainisha ipasavyo jinsi vijana wanaweza kupata Ardhi.
Mkutano huo wa nne unafanyika kuanzia leo na mingine ilifanyika nchini Benin mara mbili,na wa mwisho ulifanyika nchini Senegal.
Vijana zaidi ya 500 kutoka pande zote za bara la Afrika wanashiriki mkutano huo, wenye malengo ya kubadilishana maarifa na uzoefu na ushirikiano katika masuala ya Utawala na haki ya Ardhi kwa vijana barani Afrika.