Dkt Anthony Mveyange akizungumza katika ufunguzi wa wiki ya Azaki katika ukumbi wa kituo cha mikutano cha Kimataifa AICC Jijini Arusha |
Washiriki wasikiliza hotuba ya ufunguzi |
Na Seif Mangwangi, Arusha
Asasi za kiraia na taasisi za serikali zimetakiwa kuwekeza zaidi kwa vijana kutokana na ongezeko la changamoto zinazolikabili kundi hilo muhimu ikiwemo ukosefu wa ajira.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa kongamano la wiki ya Asasi zisizo za Kiserikali (Azaki), linaloendelea Jijini Arusha, Dk, Anthony Mveyange, Mkurugenzi wa Taasisi ya Masuala ya Kijamii ya Utawala Bora Afrika (PASGR) amesema pamoja na jitihada nyingi zinazofanyika na Serikali zetu, bado ukosefu wa ajira kwa vijana umekuwa ni tatizo kubwa.
Amesema vijana wanatakiwa kupewa vipaumbele katika mambo mbalimbali ili waweze kupata ajira kwa lengo la kujikwamua kiuchumi badala ya kuachwa wakiendelea kuzagaa mitaani wakisubiri ajira ilhali wanaweza kujiajiri wenyewe endapo wakiwezeshwa.
Dkt Mveyange amesema endapo vijana wakiwezeshwa wataondokana na changamoto mbalimbali na kuanza kubuni mbinu za kujipatia vipato kupitia kwenye azaki na makundi mbalimbali yanayojitokeza kwaaajili ya kuwapa mbinu za kujikwamua kiuchumi
Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Foundation for Civil Society(FCS),Dk,Stigmata Tenga alisema mfumo wa maendeleo unafaa kuzingatiwa na asasi hizo ikiwemo kumjali mwananchi kwanza kabla ya taasisi za umma au za kiraia.
Amesema asasi hizo zinatakiwa kuweka dira na mipango thabiti ya kubadili mfumo wa maendeleo kwa wananchi na jamii kwa ujumla ikiwemo kuangalia sera na mifumo wezeshi.
“Asasi zina wajibu wa kuhakikisha wanaangalia mifumo mbalimbali inayowaongoza ambayo ndiyo miundombinu ya uwajibikaji katika kazi zao hususani katika kutatua matatizo ya wananchi,”Amesema na kuongeza:
“Sisi tuna nguvu kubwa sana ya kuleta mabadiliko nchini,asasi za kiraia zina nafasi kubwa sana ya kuleta mabadiliko nchini kwa sababu ni sauti ya mwananchi kwanza,tuna nguvu ya kusaidia kubadilishwa sheria mbalimbali zinazowabana sekta binafsi na zinatubana na sisi kwenye ku molibize ndani na nje,”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya Help to self ,Amani Golugwa,amesema asasi za kiraia zina nafasi kubwa sana na wajibu mkubwa wa kufanya pale ambapo serikali haijafika au haijafanya.
“Sisi tumejikita kwenye elimu ya ujuzi,tunaamini ili kupambana na tatizo la ajira changamoto ya ajira kwa vijana ambao ndiyo wengi,ukimpa mtu ujuzi unakuwa umetatua tatizo la ajira,”amesema