Bandari ya tanga yavutia nchi za rwanda na burundi, zaanza kupitisha mizigo yake

Msemaji wa Bandari ya Tanga, Peter Milanzi akizungumza na waandishi wa habari  Mkoa wa Arusha kuhusu maendeleo ya bandari hiyo kongwe nchini baada ya kukarabatiwa upya.

 Na Seif Mangwangi,Arusha

NCHI za Burundi na Rwanda zimeanza kutumia bandari ya Tanga kupitishia mizigo yake kutokana na maboresho ya bandari hiyo yanayoendelea ya upanuzi wa bandari hiyo, huku nchi nyingi zaidi zikitarajiwa kutumia bandari hiyo.


Nchi ya Rwanda ambayo ilikuwa ikitumia bandari zingine kupitishia mizigo yake imeanza kutumia bandari hiyo kupitishia malighafi inayotumika kutengenezea saruji huku nchi ya Burundi ikipitisha mzigo wa mafuta kupitia bandari hiyo.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini hapa, Msemaji wa bandari hiyo, Peter Milanzi amesema kufuatia maboresho hayo yanayoendelea katika mwaka wa fedha 2021/22 bandari hiyo imefanikiwa kuhudumia mizigo tani 867,000 kutoka tani 750,000 na kwamba matarajio ni kupitisha mizigo tani milioni3 kwa mwaka baada ya kukamilika kwa mradi wote wa maboresho ya bandari.


“Wakati maboresho haya yakiendelea kwa mwaka wa fedha 2021/22 bandari yetu imeweza kuhudumia mizigo tani 867,000 na  baada ya maboresho kukamilika bandari itakuwa na uwezo wa kuhudumia shehena ya mizigo milioni 3 kwa mwaka,”amesema.

 

waandishi wa habari wakimsikiliza msemaji wa bandari ya Tanga, Peter Milanzi

“Pamoja na bandari yetu kuhudumia zaidi mizigo ya mikoa ya kanda ya kaskazini yaani Tanga,Arusha,Manyara na Kilimanjaro,nchi jirani kama Burundi na Rwanda nazo zimeanza kupitisha mizigo yao kwa wingi,”. 


“Ni matarajio yetu kuwa awamu ya pili ya uboreshaji na upanuzi wa bandari yetu ukikamilika baadaye mwaka huu,tutakuwa na uwezo wa kuhudumia watu wengi zaidi na utoaji wa huduma bora kwa wateja wetu utaboreka zaidi,” alisisitiza Milanzi katika mkutano huo wa kuhamasisha wafanyabiashara kutumia bandari hiyo.


Aliongeza kuwa uboreshaji na upanuzi wa awamu ya kwanza wa bandari hiyo ulihusisha uchimbaji wa kina cha maji kwenye mlango wa kuingilia meli na sehemu ya kugeuzia meli kutoka mita tatu hadi 13 pamoja na ununuzi wa mitambo mipya na ya kisasa ya bandari.

 

Kabla ya upanuzi huo meli zilikuwa zinatia nanga umbali wa kilimota 1.7 kutoka gati la  bandari kutokana na kina hicho kifupi cha mita tatu hatua iliyosababisha mizigo na shehena  kuhamishwa mara mbili na kuongeza gharama zisizo za lazima.

 

Kuhusu ujenzi wa Bandari kavu katika eneo la Malula wilayani Arumeru,Mhandisi wa Bandari hiyo, Hamis  Kipalo amesema kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetenga bajeti ya fedha ya kufanya upembuzi yakinifu katika mwaka huu wa fedha 2022/23.

 

“ Baaada ya upembuzi yakinifu kukamilika ndio tutajua ndio tutajua design na bajeti nzima ya mradi huo na hilo litafanyika baada ya taratibu zote za kisheria, ikiwa ni pamoja kutangaza zabuni. Bahati nzuri bajeti imetengwa mwaka huu,”amesisitiza Mhandisi Kipalo.