Dc apiga marufuku mifugo kuingia wilaya kilombero

 

Na Dismas Lyassa, Ifakara

SERIKALI wilayani Kilombero, mkoani Morogoro imeagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha hakuna mifugo mipya inayoingia wilaya humo ikiwa ni hatua za awali za kulinda Bonde la Kilombero linaloonekana kuharibiwa vibaya kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu.

Maji yanayotoka Bonde la Kilombero yanachangia asilimia 62.5 ya maji yote ya mto Rufiji ambayo ndiyo chanzo cha maji kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, hivyo uharibifu wa bonde hilo utaathiri mradi huo wa mabilioni ya fedha na maendeleo mengine muhimu ya  Taifa.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hanji Yusuph Godigodi, akizungumza na mwandishi wetu  alisema, baadhi ya mifugo imekuwa ikionekana karibu na kingo za mto Kilombero, wakulima wakiendesha shughuli za kilimo na wavuvi kujenga kambi zao katika bonde hilo kitendo ambacho kinaharibu mazingira ya bonde hilo muhimu kwa taifa.

Licha ya kusema kuwa hana idadi halisi ya mifugo iliyopo, alikiri kuongezeka kwa mifugo inayoingia kinyemela wilayani humo hasa nyakati za usiku. 

“Tumejipanga kwa hilo, hivi karibuni tulikamata mifugo kadhaa katika kijiji Iduhindembo ikiingia kinyemela katika wilaya yetu,” alisema mkuu huyo wa wilaya na kuongeza kuwa maamuzi juu ya mifugo iliyoko yatatolewa baada ya kukamilika zoezi la utumbuzi wa mifugo linaloendelea wilayani humo.

“Ukweli ni kwamba mifugo imekuwa mingi mno, hii inasababisha kutokea kutoelewana baina ya wafugaji na wakulima,” alisema Hanji.

Alipoulizwa inakuwaje mifugo inaonekana kuendelea kuingia huku ikionekana wazi kwamba eneo ni kama limezidiwa na wingi wa mifugo, mkuu huyo wa wilaya alisema tatizo sio ofisi yake isipokuwa vijiji na kata ndivyo vinavyoandika barua kwake vikieleza kwamba bado wanayo maeneo kwa ajili ya wafugaji.

“Haturuhusu tu wafugaji, bali huwa tunapokea barua za muhtasari kutoka kwenye vijiji na kata zikieleza kwamba wananchi wamekubali mifugo iendelee kuingia kwenye maeneo yao,” alifafanua kiongozi huyo.

Aidha alisema baadhi ya watendaji wa serikali za vijiji na kata wamekuwa wakipokea wafugaji wavamizi, ofisi yake inafuatilia suala hili.

Hata hivyo viongozi wa vijiji na kata wanapingana na kauli hii wakisema wao hupokea mifugo kwa maagizo kutoka juu. 

Wakasisitiza kuwa wao kama viongozi wa vijiji na kata hawana mamlaka ya kuruhusu au kutoruhusu mifugo, bali wenye mamlaka ni wilaya ambao ndio wanaotoa ruhusa kwa mifugo kuendelea kuingia kwa makubaliano wanayoyajua wao.

Diwani wa kata ya Mofu, Greyson Mgonela alisema vijiji na kata hazina mamlaka ya kuingiza mifugo, bali wenye mamlaka ni walio juu.

“Kuna wakati Mkuu wa wilaya alikuja katika mkutano na wananchi na kutulaumu sisi viongozi wa vijiji na kata, hiyo sio kweli. Sisi viongozi wa kata na vijiji hatuhusiki na hili, wenye mamlaka ni wenzetu wa ngazi za juu,” alisema na kuongeza ni muhimu kunapokuwa na tatizo kuzungumza kwa pamoja na kuona namna gani tunapata suruhu badala ya kutupiana mpira.

Kumekuwa na operesheni kadhaa ambazo zimekuwa zikiendeshwa kwa mafanikio. Hata hivyo baadae mifugo hurejea upya. Kwa mfano mwaka 2002, katika operesheni maalumu iliyoendeshwa katika bonde la Kilombero Serikali ilifanikiwa kuondoa mifugo zaidi ya 450,000, sasa imebainika mifugo inaingizwa tena kwa wingi.

Bonde la Kilombero lilitengwa kuwa Pori Tengefu kwa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura ya 302 ya mwaka 1952 (Fauna Conservation Ordinance CAP 302 of 1952 GN.No.107) likiwa na ukubwa wa km za mraba 6,500. 

Sababu kubwa ya Serikali kufanya hivyo ni kutokana na ukweli kuwa Bonde lilionekana kuwa na umuhimu wa kimataifa na kuorodheshwa kuwa eneo la Ramsar (eneo linalopaswa kutunzwa na kulindwa tarehe 24/04/2002 na kupewa namba 1173 (W1 ItZ03).

Hata hivyo uchunguzi unaonyesha licha ya kuwa na maagizo na maelekezo mengi ya kutaka bonde hilo lilindwe, shughuli za kibinadamu zinaendelea kwa kasi katika bonde la Kilombero hali inayosababisha baadhi ya wananchi na wadau wa mazingira kumuomba rais kuingilia kati.

Wananchi wengi wanapendekeza ofisi ya Rais au waziri mkuu kuinuka kuja kuingilia suala la bonde la Kilombero kwani kadri miaka inavyokwenda mbele linazidi kuharibiwa. 

”Sote tunajua umuhimu wa bonde hili, lakini kadri miaka inavyokwenda mbele linazidi kuharibiwa,” alisema James Lingwa ni mkazi wa Lipangalala, Ifakara.