Wajumbe mabaraza ya ardhi watakiwa kuacha rushwa

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda akimkabidhi mwenyekiti wa baraza la kata ya Olasiti Adam, vitendea kazi

 Na Seif Mangwangi, Arusha

Wajumbe wa mabaraza ya kata wametakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kuwa wameaminiwa na  kuchaguliwa kwaajili ya kutoa haki na sio kupindisha haki za watu.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda katika hotuba yake ya uzinduzi wa mabaraza ya kata na ufunguzi wa mafunzo kwa wajumbe wake kutoka katika kata 25 za Jiji la Arusha.

Amesema kazi ya wajumbe ni kutoa haki ” Nasisitiza sana huna haja ya kula rushwa, ukifanyakazi vizuri utapewa takrima na wale uliowapa haki watakuombea dua njema ili ifanikiwe, mioyo ya watu uliowafanyia mambo mazuri na yenyewe inakuwa mizuri na wewe unabarikiwa”Amesema.

DC Mtanda amesema hakuna mtu ambaye anaweza kutajirika kwa kula rushwa kwa kuwa hakuna haramu inayodumu na kwamba hata kama utanunua vitu vingi mwisho wake vitapukutika.

Amesema pamoja na kuundwa kwa mabaraza hayo kisheria, bado yanaweza kuvunjwa endapo wajumbe wake wataonekana wanaenda kinyume na matakwa ya mabaraza hayo.

DC Mtanda amesema Serikali inaangalia namna ya kuyawezesha mabaraza ya Ardhi kwa vifaa na fedha ili wajumbe waweze kupata posho ya kujikimu kwa kuwa yamekuwa yakifanya kazi kwa kujitolea.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo amesema sheria za mabaraza zimepitwa na wakati hasa katika kipengele cha faini kwa wale ambao wamekuwa wakidharau mabaraza ambapo sheria inasema mtu akidharau baraza anapaswa kutozwa faini ya TZS 400 pekee fedha ambayo ni ndogo.

Mwanasheria wa Jiji Iddi Ndabhona akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mafunzo waliyotoa kwa wajumbe wa mabaraza ya kata Jiji la Arusha

Mwanasheria wa Jiji Iddi Ndabhona amesema wametoa mafunzo kwa lengo la kuwakumbusha wajibu wajumbe wa mabaraza ya kata lakini pia kusisitiza wajumbe wa mabaraza hayo kuwa haki waliyopewa ya kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi imeshaondolewa na hivi sasa wamebakia kwenye usuluhishi pekee.

Amesema kikubwa ambacho mabaraza ya kata yameendelea kusikiliza ni migogoro ya ardhi na kutolea maamuzi, jambo ambalo limekuwa likileta ukakasi katika utekelezaji wa hukumu wanazotoa.

” Tunawasisitiza wasiwe kikwazo kwenye utatuzi wa migogoro unakuta mtu anapeleka malalamiko yake wanakaa na kesi za watu badala wawaeleze pa kwenda wanaendelea kukaa nayo,”amesema.

Amesema sheria ya mabadiliko ya sheria namba3,2021 imefanyia mabadiliko ya sheria ya mabaraza baada ya kugundua kuwa wamekuwa wakitumia mamlaka waliyokuwa nayo kama mahakama jambo ambalo sio sahihi.

Mohamed Abdallah Ally mjumbe wa baraza la kata ya  unga ltd amesema vitendo vya rushwa katika mabaraza ya kata vimekuwa vikichangiwa na ukosefu wa posho za mabaraza hali ambayo imekuwa ikiwalazimu kuwatoza fedha walalamikaji wanaofikisha mashauri yao katika baraza.

Ameiomba Serikali kuwapatia posho ili kuweza kuondokana na hali hiyo na kuacha kuwatoza fedha watu ambao wamekuwa wakifikisha malalamiko yao katika mabaraza hayo.

Mzee Yeremia Mwanga mjumbe wa baraza la kwa Maganga Morombo amewataka wajumbe wenzake kuwapenda wananchi na kusaidia badala ya kudai rushwa kupitia mabaraza hayo jambo ambalo sio sahihi.

Wajumbe wa Baraza la kata wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda (hayupo pichani)