Iran yasitisha utekelezaji wa makubaliano wa nyuklia ya mwaka 2015

Serikali
ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo Jumatatu imetoa
taarifa ikitangaza kuwa imechukua hatua ya tano na ya mwisho ya
kupunguza utekelezaji wa ahadi zake katika makubaliano ya nyuklia
maarufu kwa kifupi kama JCPOA.


Taarifa
hiyo imesema kuwa, kuanzia sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitakuwa
na kizuizi chochote katika shughuli zake za nyuklia ikiwa ni pamoja na
kurutubisha madini ya urani, asilimia ya urutubishaji wa madini hayo,
kiwango kinachorutubishwa na katika masuala ya utafiti na uchunguzi.

Kwa
msingi huo katika hatua hii ya tano, Iran imetupilia mbali kizuizi
muhimu zaidi cha shughuli zake kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya
JCPOA ambacho kinahusiana na idadi ya mashinepewa zinazoruhusiwa kufanya
kazi.

Iran
imesema katika taarifa hiyo kwamba, tokea sasa miradi yake ya kuzalisha
nishati ya nyuklia itafanya kazi kwa mujibu wa mahitaji yake ya
kiufundi. 

Imesisitiza
kuwa, Iran itaendelea kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya
Atomiki (IAEA) na kwamba iwapo vikwazo vyote vitaondolewa na Tehran
ikafaidika na maslahi ya JCPOA,  iko tayari kutekeleza tena vipengee vya
makubaliano hayo.