Serikali kufuta vyama 3,436 vya ushirika

Serikali 
inakusudia kuvifuta vyama vya ushirika vipatavyo 3,436 ambavyo
vimeshindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi na havipatikani huku
vingine vikiwa havijulikani vilipo.


Kwa
kuzingatia matakwa ya sheria no 6 ya mwaka 2013 ya vyama vya ushirika
kifungu 100 na kanuni ya 26, Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga
amemuagiza Mrajisi wa vyama hivyo kutoa notisi ya siku 90 kwenye gazeti
la serikali ya kusudio la kuvifuta.

Akizungumza
na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma jana, Mhe Hasunga
amesema asilimia kubwa ya vyama vilivyokusudiwa kufutwa ni vyama vya
ushirika wa akiba na mikopo ambavyo ni asilimia 73.8.

Amesema
vyama hivyo vingi ni matokeo ya mfumo wa uwezeshaji wa wananchi
kiuchumi ujulikanao kama Jakaya Kikwete Fund ambao ulilenga kuwawezesha
wananchi kiuchumi.


Katika mpango huu wa JK Fund wananchi wengi walianzisha SACCOS kwa
lengo la kupata mikopo kutoka kwenye mfuko huo, Aidha vyama ambavyo
havikupata mkopo havikuendelea na majukumu yake na hata vilivyopata
mikopo baada ya kupata walitelekeza vyama hivyo jambo linalopelekea kuwa
na SACCOS nyingi hewa,” Amesema Mhe Hasunga.

Amevitaka
vyama ambavyo orodha yake itapatikana kwenye tangazo la mrajisi
litakalotolewa kwenye gazeti la serikali, mtandao wa wizara ya kilimo na
mtandao wa Tume ya Ushirika kujitokeza na kutoa sababu za kwanini
wasifutwe kwenye orodha ya vyama vya ushirika.


Tunavitaka vyama vyote vya ushirika nchini kuendesha shughuli zao kwa
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Vyama vyote vinatakiwa
kuwahudumia wanachama wake na siyo vinginevyo,” Amesema Mhe Hasunga.

Mhe
Waziri amesema mpaka sasa daftari la mrajisi wa vyama vya ushirika lina
jumla ya vyama 11,149 vilivyoandikishwa kati ya vyama hivyo, 3,436
havijulikani vilipo, vyama 1,250 vimesinzia na vyama 6,463 vipo hai.

Amesema
sababu zinazopelekea kufutwa kwa vyama hivyo ni kushindwa kuwa na ofisi
huku viongozi wake wakiwa hawajulikani, Chama kushindwa kufanya
shughuli zake ndani ya miezi sita tangu kiandikishwe pamoja na idadi ya
wanachama kupungua kwa mujibu wa mahitaji ya kisheria.

Sababu
nyingine ni vyama hivyo kushindwa kutekeleza takwa la kisheria la
kutayarisha makisio ya mapato na matumizi na kuyapeleka kwa mrajisi
kuyapitisha, kutayarisha taarifa ya mwaka, kufunga mahesabu na
kuyapeleka COASCO kwa ukaguzi, kutofanya mikutano ya mwaka ya wanachama
na bodi zao.

Katika
orodha ya vyama vya ushirika kimkoa vinavyokusudiwa kufutwa kwenye
daftari la mrajisi wa vyama, Mkoa wa Mwanza unaongoza ukiwa na jumla ya
vyama 393, Pwani ya pili yenye vyama 335 huku Kagera ikishika nafasi ya
tatu kwa vyama 301.

Kwa
upande wake Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Dk Benson Ndiegi
amesema serikali haitowavumilia viongozi wa vyama ambavyo vitakaidi
maagizo hayo yaliyotolewa na Mhe Waziri.


Baada ya agizo hili la Mhe Waziri na baada ya kutoa notisi hizo kwenye
gazeti la serikali tutakua tayari kupokea maelezo na taarifa kutoka
kwenye vyama na wale ambao watakua wanafutwa waje na wanaamini wana
nafasi ya kuendelea kuwepo inabidi waje na vielelezo vyao,” Amesema Dk
Ndiegi