Itcoeict ya dit yazindua mafunzo ya tehama kwa walimu

 KATIKA kuendana na mabadiliko ya TEHAMA, Taasisia Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kupitia Kituo cha umahiri wa TEHAMA (ITCoEICT) itakua na mafunzo ya siku tano kwa walimu wa shule za msingi na sekondari zaidi ya 300 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini katika mafunzo yaliyofadhiliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

 

Mafunzo hayo ya siku tano yamefunguli na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makanza huku ikielezwa kuwa lengo la mafunzo hayo yanayojulikana kitaalamu kama ‘Basic ICT Devices Maintenance and Repair’ ni kuimarisha utunzaji wa vifaa vya TEHAMA ambavyo hutolewa na serikali na wadau wengine kwa shule mbalimbali nchini.

 

Vifaa hivyo ni pamoja na kompyuta, printa na vifaa vya mawasiliano kupitia UCSAF. Mafunzo hayo hutolewa kwa walimu hao baada ya kuonekana kuwa ni muhimu vifaa hivyo vikatunzwa.

 

Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Profesa Preksedis Ndomba katika tukio la ufunguzi wa mafunzo hayo, anasema walimu hao wako sehemu sahihi kabisa katika kupata mafunzo hayo.

 

“DIT ni Taasisi mahiri katika TEHAMA na hivyo mpo mahali sahihi kabisa, niwataarifu tu kuwa pamoja na umahiri huo, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kulitambua hilo imeidhamini Taasisi yetu kupata mkopo wa Benki ya Dunia kujenga Kituo kikubwa cha Kikanda cha Umahiri wa TEHAMA kijulikanacho kama RAFIC.

 

Alisema DIT inafanya jitihada mbalimbali katika kuinua elimu ya ufundi na teknolojia nchini ambapo imeandaa maandiko kadhaa ya miradi na kufanikiwa kupata ama ufadhili au mikopo yenye masharti nafuu kwa madhumuni ya kutumia vizuri wataalam waliopo katika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii yetu ya Tanzania.

 

 

Aidha, Profesa Ndomba alisema anaamini kuwa mafunzo bora ya TEHAMA watakayoyapata yatawezesha kufikiwa malengo kusudiwa kwa manufaa ya Taifa na wao binafsi kupata ujuzi na utaalam wa kuimarisha utunzaji wa vifaa vya TEHAMA ambavyo hutolewa na Serikali na wadau wengine wa maendeleo kwa Shule mbalimbali nchini.

 

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kituo cha Umahiri wa TEHAMA (ITCoEICT) kilichopo DIT, alisema mafunzo hayo yanatolewa pia Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo kikuu cha technolojia na Sayansi cha Mbeya (MIST) yakiratibiwa na DIT. Mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo  walimu kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya kisasa.

 

 

Aidha, anasema DIT inaunga mkono mikakati ya serikali ya awamu ya tano chini ya Mh. Daktari John Joseph Pombe Magufuli ambayo ina nia ya dhati ya kuboresha elimu sambamba na kuwasaidia walimu katika mafunzo haya ya TEHAMA kwa walimu wa shule za serikali nchini.

 

DIT inatoa wawezeshaji, vifaa pamoja na miundombinu mingine kwa ajili ya kufanikisha mafunzo haya muhimu.

Mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo  walimu kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya kisasa.