Jafo atoa maelekezo kwa rc mtaka, ni kuhusu kuibiwa kwa ultra sound

Na Mwandishi Wetu, APC BLOG DODOMA

SIKU mbili baada ya mashine ya Ultrasound kuibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe Suleiman Jafo amemtaka Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka kuunda tume maalum ya kuchunguza tukio hilo.

Mashine hiyo inadaiwa kuibiwa pamoja na kifaa chake cha kudurufu picha (printer) ambapo ilikua maalumu kwa matumizi ya wodi mpya ya akina Mama wajawazito na iliibiwa ikiwa katika wodi hiyo.

Akizungumza jijini Dodoma, Waziri Jafo amesema hajafurahishwa na kitendo cha mashine hiyo kuibiwa kwa sababu kinarudisha nyuma maendeleo makubwa ambayo Serikali imeyafanya katika sekta ya Afya nchini.

” Kitendo cha mashine hii kuibiwa kinaonesha jinsi gani wapo watu wenye nia ovu ya kurudisha nyuma Uwekezaji ambao Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeufanya katika sekta ya afya, sasa nitoe maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa kuhakikisha anatuma Timu ya kwenda kuchunguza ili tujue mashine hiyo iliibiwaje,”amesema Waziri Jafo.

Aidha ametengua kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi aliyoagiza watumishi 137 wa Hospitali hiyo kuchangia kutoka kwenye mishahara yao ndani wiki moja ili kulipa machine hiyo iliyoibiwa.

” Maelekezo yangu ni kwamba kutokana na hali iliyojitokeza huko Timu itakayoundwa kuchunguza tukio hilo inapaswa ije na majibu ambayo tutawajua waliofanya wizi huo ambapo kwanza watapaswa kurudisha mashine hiyo kisha wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kupandishwa mahakamani.

” Kuhusu watumishi 137 kulipia mashine hiyo kutoka kwenye mishahara yao, nielekeze kuwa watumishi hawa wanafanya kazi kwenye mazingira magumu kitendo cha kuwaambia walipe ni kuwakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma,” amesema Waziri Jafo.

Amezitaka mamlaka za Wilaya ya Bariadi kutowachangisha fedha watumishi hao na badala yake wajielekeze katika kuhakikisha wanawapata waliohusika na wizi huo ili wachukuliwe hatua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *