Lhrc yatoa wito kwa azaki kusaidia wananchi mabadiliko ya tehama

Anna Jenga, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha misaada wa Kisheria Tanzania (LHRC)

Na Cynthia Mwilolezi, ARUSHA 

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga  ameziomba Asasi za kiraia nchini,  kuhakikisha zinasaidia watu kuendana  na mabadiliko  ya  teknolojia  (TEHAMA) ili kuleta matokeo chanya ulimwenguni.

Anna Henga alitoa ombi hilo jana jijini hapa katika mkutano ulioandaliwa na kituo cha sheria nchini (LHRC), ikiwa ni  muendelezo wa shughuli zinazoendelea katika maadhimisho ya wiki ya Azaki  inayofanyika katika kituo cha mikutano cha AICC jijini Arusha. 

Alisema Dunia inabadilika kwa kasi sana na hivyo kila mtu anapaswa kubadilika ili kuendana na mabadiliko hayo ya kiteknolojia na kwamba ili kuwa sawa asasi za kiraia zinapaswa kubadilisha wadau wao  bila kubagua wasomi na wenye uwezo.

“Nawaomba Azaki tubadilike tuendane na mabadiliko ya TEHAMA ili Teknolojia hii isituache nje na tunapobadilika tubadilike na watu wote bila kubagua  watu  ili kuleta matokeo chanya katika jamii,”alisema.

Alisema Azaki zimekuwa zikifanya kazi kubwa katika jamii na kusema kwa pamoja na kazi hizo, asasi hizo zinapaswa kuendelea  kusaidia watu katika upatikanaji wa haki za kiuchumi,kiraia,kusikilizwa na nyingine nyingi.

Aidha, alisema haki ya kusikilizwa muhimu na ili mtu aweze kupata huduma  za kijamii ni lazima asikilizwe.

Pia alizitaka asasi hizo kuitambua fedha sio msingi wa maendeleo bali lazima wananchi wakubali koke kitu wanachokiamini watatoa ushirikiano.

“Mfano mradi ukiendelea katika jamii yao wananchi wapo tayari kujitolea kwa hali na mali ikiwemo  fedha na hata ikitokea mfadhili amejiondoa mradi utaendelea sababu wananchi wameshirikishwa  na wameona kile kinachofanyika ni chao,”alisema.

Alihimiza katika utawala bora, umuhimu wa kuandaa vijana kwenye utendaji kazi wao, maana wao ni wepesi katika mabadiliko ya Teknolojia tofauti na mtu mzima, kadri umri unavyokùwa mkubwa mambo mengi yanamtupa nje.