Lishe duni yaendelea kuisakama halmashauri ya wilaya ya singida…

Mtoto akifurahia uwepo wa vyakula mbalimbali vinavyotakikana kwenye Lishe bora

 Ijumaa, Desemba 29, 2023

Na Abby Nkungu, Singida

 

TATIZO la lishe duni bado ni changamoto katika halmashauri ya wilaya ya Singida ambapo takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa asilimia 20 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na udumavu.

Mbali na udumavu, takwimu hizo zinazoishia Desemba mwaka jana 2022 kutoka idara ya lishe katika halmashauri hiyo pia zinaonesha kuwa asilimia 8 ya watoto wa umri huo wana uzito pungufu na asilimia 2 wana ukondefu.

Afisa lishe katika halmashauri hiyo, Edes Peter anasema licha ya Wilaya hiyo kuwa moja ya wazalisha wakubwa wa vyakula; hasa vya asili, lakini tatizo ni elimu duni kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya lishe bora kwa watoto hali inayosababisha kuwepo kwa udumavu, uzito pungufu na ukondefu kwa kundi hilo.

“Singida tuna kuku wengi wa asili na mazao yake, mbuzi, viazi vitamu, mafuta ya alizeti nk lakini tatizo ni uelewa duni tu. Hata hivyo, tunamshukuru Mungu kwamba hivi sasa kuna Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto iliyoanza kutekelezwa Januari mwaka 2021hadi mwaka 2026 ambayo inashughulika na mambo yote muhimu kwa mtoto” anasema.

Edes anaeleza kuwa chini ya Programu hiyo, wadau mbalimbali  wamekuwa wakiunganisha nguvu kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kuimarisha lishe kwa watoto walio na umri wa miaka 0 hadi 8, afya bora, Malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji wa awali na ulinzi na Usalama kwa kundi hilo muhimu katika jamii.

Vyakula muhimu vinavyoshauriwa na wataalamu katika kukamilisha Lishe bora

“Pamoja na elimu ya lishe kupitia Programu hiyo, Serikali kwa upande wake imeongeza bajeti ya lishe kwa mtoto kwa kila  halmashauri kutoka 1,000/- kwa mwaka 2020/21 hadi 1,239/- kwa mwaka 2021/2022, zinafika kwa walengwa na kutumika ipasavyo” alifafanua.

Ingawa Afisa lishe huyo anasema zipo hatua zinazochukuliwa kumaliza tatizo hilo, wataalamu wa afya ya mama na mtoto wanataka tatizo la udumavu, ukondefu na uzito pungufu kuwekewa mkakati wa kutokomezwa haraka, kwani hilo ni miongoni mwa sababu za homa za mara kwa mara kwa watoto.

“Lishe duni ni chanzo mojawapo cha magonjwa na vifo kwa watoto wadogo hasa walio chini ya miaka mitano. Pia, hudumaza ukuaji wa kimwili na kiakili na hupunguza uwezo wa mtoto kufanya vizuri shuleni na hata ufanisi wa kazi katika maisha ya utu uzima”, anaeleza  Dk Suleiman Muttani, Daktari Bingwa Mshauri Mwandamizi  wa magonjwa ya Wanawake na Watoto katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida.

Hata hivyo,  wadau wengine wakiwemo wazazi, walezi na wataalamu kutoka masharika, asasi za kiraia na  taasisi zinazoshughulikia ustawi wa mtoto wanasema njia pekee ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa lishe bora kwa mtoto  ndani ya siku 1,000 za awali ili kujenga afya bora.

“Unaweza kushangaa kuwa tatizo kubwa la lishe duni kwa watoto lipo vijijini kuliko mjini wakati huko ndiko vyakula vingi vya asili na vyenye virutubisho vinapatikana na kuletwa hapa mjini kuuzwa.  Kwa hiyo, shida kubwa ni elimu kwa jamii” anasema Evarista Lucas mkazi wa Soko la vitunguu Singida na kuungwa mkono na Joshua Ntandu, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la ESTL linalotekeleza Programu Jumuishi ya Taifa – Malezi, Makuzi na maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) mkoani Singida.

Joshua anasema kuwa pamoja na elimu duni ya lishe, tatizo lingine ni imani potofu miongoni mwa jamii hasa vijijini juu ya ulaji wa baadhi ya vyakula muhimu vinavyoshauriwa na wataalamu wa afya na lishe ili kujenga mwili wa mama mjamzito na mtoto mara baada ya kuzaliwa

“Huwezi amini ila kwa hakika ukitoka nje ya mji kidogo tu kuna wajawazito na watoto  ambao  hawali mayai, maini, firigisi na vyakula vingine vingi muhiumu eti kwa ushauri wa wazee. Hii inaturudisha nyuma kabisa katika suala la lishe bora” anasema Joshua.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua  mbalimbali timilifu za ukuaji kutokana na  kuwepo kwa viashirikia vya utapiamlo, umasikini na kukosekana kwa uhakika wa chakula