Mahakama ya afrika yawataka waandishi wanawake kuonyesha umahiri ili kufuta dhana ya mfumo dume

Rais wa Mahakama ya Afrika ya watu na Haki za binaadam, Jaji Imani Aboud (katikati aliyekaa), akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari Wanawake pamoja na watendaji wa baraza la Habari nchini

 Na Seif Mangwangi, Arusha

WAANDISHI wa habari Wanawake wenye nafasi mbalimbali za uongozi kwenye vyombo vya habari nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu,weledi na kujiamini ili kuondoa dhana ya mfumo dume ambao umeendelea kuwepo kwa miaka mingi.

Wito huo umetolewa Jana Juni21,2023 na Rais wa Mahakama ya Afrika ya watu na Haki za binaadam (AfCHPR), Jaji Imani Daudi Aboud alipokuwa akifunga  mafunzo ya siku tatu ya uongozi kwa baadhi ya waandishi wa habari Wanawake nchini yaliyokuwa yakiendelea Jijini hapa.

Jaji Imani amesema kwa kipindi kirefu sekta ya habari nchini imekuwa na wanaume zaidi na tafiti mbalimbali zilizofanywa zimethibitisha kuwa wanaume wameendelea kuhodhi madaraka katika vyombo vya habari.

Amesema  pia maudhui ya vyombo hivyo bado hayajazingatia vya kutosha sauti za wasio na sauti ikiwa ni pamoja na wanawake na makundi mengine ya pembezoni.

” Utafiti uliofanywa na Baraza la Habari Nchini mwaka 2019,  umethibitisha bado kuna upungufu katika nafasi za uongozi , hivyo mafunzo haya yatakuwa ni dira ya kupata viongozi mahiri wanawake katika vyombo vya habari ambao watachangia kuleta mabadiliko katika sekta ya habari,” amesema.

Amewataka waandishi wa habari wanawake waliopata nafasi hiyo ya mafunzo kufanyakazi kwa bidii, ubunifu, weledi na kijiamini na kwamba kwa kufanya hivyo wataweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu.

Awali akimkaribisha Jaji Aboud, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga amesema Baraza kupitia Moja ya programu zake imekuwa ni kutoa elimu ya uongozi kwa waandishi wa habari Wanawake na Hadi kufikia Juni mwaka huu tayari waandishi wa habari Wanawake 128 wameshapatiwa mafunzo.

Mukajanga amesema matokeo ya mafunzo hayo ni makubwa kufuatia wengi wa waliopata elimu hiyo wameweza kuonyesha umahiri kwenye utendaji wa kazi Hadi kupewa uongozi.

” Mheshimiwa Jaji huu utaratibu wa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari Wanawake tumeanza miaka mitano iliyopita na matokeo yake yamekuwa makubwa sana ambapo wengi tuliowapatia mafunzo hivi sasa ni viongozi kwenye vyombo vyao vya habari wanavyofanyia na wamekuwa wakifanya vizuri sana,” amesema.

Elizabeth Mramba mkuu wa Kanda wa shirika la utangazaji TBC, akipokea cheti kutoka kwa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binaadam, Jaji Imani Aboud baada ya kuhitimu mafunzo ya uongozi ya siku tatu
Mwandishi wa habari mwandamizi na mwanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Arusha Veronica Mheta akipokea cheti kutoka kwa Rais wa Mahakama ya Afrika ya watu na Haki za Binaadam Jaji Imani Aboud baada ya kuhitimu mafunzo ya siku tatu ya uongoz