Makonda atoa onyo kwa watendaji wanaomhujumu

Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema katika kipindi cha
uongozi wake hajawahi kutoa onyo kwa njia ya barua kwa kiongozi yeyote
chini yake ndani ya mkoa huo, lakini sasa ataanza kuwashughulikia
kutokana na hujuma anazofanyiwa.

Jumapili
iliyopita, wakati wa kuwaapisha viongozi aliowateua, akiwamo Mkuu wa
Morogoro, Rais Magufuli alionyeshwa kusikitishwa na kusuasua kwa miradi
ya maendeleo ilhali mkuu huyo wa mkoa yupo.

Kutokana na madai hayo ya kuhujumiwa, Makonda ametangaza kuwa atawachongea watendaji hao kwenye ngazi za juu za utawala.

Pia
amelalamika kuwa amekuwa akitoa maagizo kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi ya maendeleo lakini badala ya kutekeleza, baadhi ya watendaji hao
wamekuwa wakitafuta uhakika kutoka kwa wakuu wa idara.

Makonda
aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na wakuu wa wilaya zote tano za
mkoa wa Dar es Salaam, wakurugenzi wa manispaa, viongozi wa jiji na
watendaji wote katika kikao cha kujadili sababu za kukwama kwa miradi
mbalimbali ya maendeleo.

“Haina
maana kama mimi natoa maagizo na nyie viongozi badala ya kuyafuata
mnaanza kupitisha vimemo kuuliza kama mtafanyaje ili kutafuta uhakika,
ina maana mkuu wa mkoa hana washauri wazuri ndio sababu ya kutofuata
maelekezo yake,” alisema Makonda.

Alimtaja
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi, ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya
ya Kinondoni kuwa alikuwa akifuata maelekezo yake bila vikwazo tofauti
na viongozi wengine walio chini yake, akiwamo anayeshika nafasi hiyo kwa
sasa. Kwa sasa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ni Daniel Chongolo.

“Nilikuwa
nikifanya vikao ofisini kwangu na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally
Hapi na wa Ilala Sophia Mjema. Walikuwa wakifuata ninachowaeleza lakini
hawa wengine kila nikiwaambia lazima waanze kupita pita na kuuliza hapa
sijamwelewa. Mnapiga majungu yenu, sasa inatosha na mimi nitaanza
kuwashughulikia,” Makonda alisema.

Alisema
viongozi na watendaji wa mkoa huo, wanapaswa kufuata maagizo yake kwa
sababu ndiye aliyepewa jukumu la kusimamia mkoa huo.

“Haijalishi
kama umenipita umri au nilikukuta serikalini lakini uko chini yangu
tu,” alisema Makonda na kuongeza kuwa ili kumaliza utata na fitina hizo,
naye atakuwa akitoa taarifa za viongozi wasiotimiza wajibu wao kwa
viongozi wa juu yake.

Alisema
pia kila maagizo atakayokuwa akiwapatia, atakuwa akituma nakala kwa
uongozi wa juu ili kuondokana na changamoto ya kuonekana mzembe ilhali
anatimiza wajibu wake.

“Tangu
nimekuwa mkuu wa mkoa huu, sijawahi kuandika barua kwa viongozi wa juu
kumsema kiongozi yeyote, awe mkuu wa wilaya au wakuu wa idara. Lakini
sasa nitaanza kuwasema. Nimeshamwambia Katibu Tawala wa Mkoa kila
ninapotoa maagizo atoe na nakala kwenda kwa viongozi wa juu,” alisema
Makonda.

Aidha,
aliwataja viongozi wa wilaya ya Kinondoni ambao mradi wa fukwe za Coco
umekwama na anapowapa maagizo hawayafuati na kusababisha mkoa kupata
sifa mbaya za kukwama kwa miradi.

“Natoa
ushauri nyie mnafuata wa kwenu. Nikiuliza mnaitisha vyombo vya habari
kusema mnafuata sheria. Mnapindua maagizo yangu na kufuata yenu.
Tusishindane, tunapozidiana madaraka kila mtu atimize wajibu wake,”
alisema.