Marekani yawataka raia wake kuondoka iraq haraka

Waziri
Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahuu ameikatiza ziara yake ya Ugiriki
kufuatia kuuawa kwa Meja Jenerali Qassem Soleimani, mkuu wa jeshi maalum
la Iran. 


Hayo ni kwa mujibu wa afisa mmoja kutoka ofisi ya Waziri Mkuu huyo. 

Netanyahu
amekuwa mjini Athens kufuatia muafaka uliotiwa saini na Ugiriki, Cyprus
na Israel hapo jana, wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asili kutoka
eneo linakopatikana mafuta la mashariki ya Mediterania hadi Ulaya.

 Redio
ya Jeshi la Israel imeripoti kuwa jeshi la nchi hiyo liko katika hali
ya tahadhari kubwa, likihofia ulipizaji kisasi wa Iran au washirika wake
baada ya kuuliwa kwa Soleimani katika shambulizi la angani mjini
Baghdad. 

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani imewataka raia wa Marekani kuondoka nchini Iraq haraka iwezekanavyo. 

Shughuli
za ubalozi wa Marekani mjini Baghdad zilisitishwa mapema wiki hii
kufuatia mashambulizi kwenye jengo la ubalozi na wafuasi wa wanamgambo
wanaoungwa mkono na Iraq.

Waziri
mkuu wa Iraq anaeondoka Adel Abdul-Mahdi amelaani mashambulizi ya
Marekani na kuitishia kikako cha dharura cha Bunge kuchukuwa kile
alichokiita hatua stahiki zinazohitajika ili kulinda hadhi, mamlaka na
uhuru wa Iraq.


Mataifa mengine pia yamezungumzia mauaji hayo ambapo Urusi imesema
yanaweza kuchochea zaidi mzozo katika kanda ya Mashariki ya Kati, huku
Ufaransa ikisema mauaji ya Soleimani hayatatuliza mzozo bali
yatauchochea zaidi.
China kwa upande wake imeomba pande zote kujizuia huku utawala wa Syria
ukilaani pia mauaji hayo uliyoyataja kama ya kiuoga kwa upande wa
Marekani.