Mbunge manyanya ataja kilichosababisha ccm kushinda kwa kishindo uchaguzi mkuu 2020

 

Na Alex Sonna, Dodoma


MBUNGE
wa Nyasa(CCM), Mhandisi Stella Manyanya, amesema sababu za Chama cha
Mapinduzi(CCM), kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu 2020 ni
kutokana na mambo yaliyofanywa na serikali chini ya Rais Dk.John
Magufuli.


Akichangia
Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Miaka mitano bungeni leo, Manyanya
amesema wananchi wameelewa namna ambavyo CCM imetekeleza yale
yaliyoahidiwa na masikio yao kwasasa wasikiliza mpango huo
utawasaidiaje.


“Mpango huu utakuwa na maana zaidi pale tutakapohakikisha unakuwa na manufaa kwa watanzania,”amesema.


Aidha,
ameishauri serikali kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa bwawa la
uzalishaji umeme la Mwalimu Nyerere na ujenzi wa reli ya kisasa katika
Mpango huo kwa kuwa miradi hiyo ni mkombozi kwa watanzania.



“Inahitaji mtu ambaye hakuwepo kwenye mgao wa umeme ashangae Bwawa la
Nyerere, ni mtu atakayeshindwa kujua tunapoteza mapato kutokana na
usafirishaji mizigo kutoa bandarini kupeleka nchi jirani, wana CCM tuna
wajibu wa kuelimisha wananchi ili kujua umuhimu wa miradi hii
mikubwa,tuendelee kuisemea hadi itakapokamilika,”amesema.


Ameomba serikali kukamilisha miradi hiyo ili isaide upatikanaji wa fedha nyingi za kuhudumia maeneo mbalimbali katika nchi.


“Tuwe na fedha kidogo au zaidi lazima miradi hii ya kimkakati ikamilike, pia tuimalishe ulinzi wa mipaka yetu,”amesema.


Aidha, amesema maendeleo yanakwenda kwa kasi Nyasa na Mbinga kutokana ujenzi wa barabara uliofanywa.


“Niombe
yale yaliyoainishwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM barabara ya
Chiwindi-Mbambay hadi Litui-Amani makoro na daraja la mitomoni kipande
kile kinadai katika mpango huu mambo yatekelezwe kama
yalivyoahidiwa,”amesema.