Mpasuko mkali wainyemelea marekani….trump agoma kumpa mkono spika, spika naye kaamua kuichana hotuba yake

Rais
Trump kususia mkono wa Spika Pelosi na Pelosi kumjibu kwa kuichana
hotuba yake ni baadhi tu ya vitimbi vilivyodhihirisha mgawanyiko mkali
wa kisiasa nchini Marekani, wakati Trump alipotoa hotuba kuhusu hali ya
nchi.

Tofauti
na ilivyozoeleka kuwa hotuba ya rais wa Marekani kuhusu hali ya nchi ni
muda wa maridhiano kisiasa, mazingira katika kikao cha Congress
kilichowaleta pamoja wajumbe wa baraza la wawakilishi na maseneta
yaliakisi mpasuko mkali wa kisiasa muda wote wa saa moja na dakika 18 wa
hotuba ya Trump.

Zoezi zima lilianza vibaya pale Rais Trump alipokataa kuupokea mkono
alionyooshewa na spika wa baraza la wawakilishi Bi Nancy Pelosi na
kuuacha ukining’inia hewani. 

Na
lilimalizika kwa hatua ya Pelosi kumjibu Trump mtindo wa jino kwa jino,
alipochana vipande vipande nakala ya hotuba ya Trump aliyokuwa
amekabidhiwa, mara tu Trump alipomaliza kuzungumza. 

Rais
Trump ametumia sehemu kubwa ya hotuba yake kwa majigambo, ya namna
alivyofanikiwa kuukarabati uchumi wa Marekani, na hadhi ya nchi hiyo,
ambavyo amedai vilikuwa vimewekwa rehani na watangulizi wake. 


Masuala
mengine aliyoyamulika Trump katika hotuba yake, ni makubaliano ya
kibiashara kati ya China, na mengine ya eneo huria la kibiashara katika
nchi za Amerika Kaskazini, akisema hayo ni mafanikio makubwa ambayo
yatarejesha maelefu ya viwanda nchini Marekani.

Amezungumzia pia sera za kupunguza kodi na kumaliza kuhusika kwa majeshi
ya Marekani katika mizozo ya Mashariki ya Kati, kama ushahidi wa
kutimiza ahadi alizozitoa kwa wapiga kura.

Hotuba yake ilishangiliwa mara kwa mara na wabunge wa chama chake cha
Republican waliosimama kumpigia makofi, huku wademocrat wakibakia katika
viti vyao, baadhi wakizomea, na wengine hata kutoka nje.