Mtoto aliwa na fisi kitangili

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mtoto Alberth Shija mwenye umri wa Miaka Miwili na miezi kumi Mkazi wa kitongoji cha  Imalilo kata ya kitangili Manispaa ya Shinyanga, amefariki Dunia baada ya kushambuliwa na fisi.

Kwa mujibu wa Mama mzazi wa Mtoto huyo Bi Elizaberth Charles tukio hilo limetokea jana majira ya saa moja  usiku, baada ya familia hiyo  kumaliza kula chakula cha usiku ndani ya nyumba yao, na baadaye  mtoto huyo alitoka nje lakini ghafla alisikia mwanaye akipiga kelele na alipotoka nje alikuta fisi amemnyakua akikimbia naye

Amesema baada ya fisi kumwachia mtoto huyo alipelekwa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga lakini alifariki Dunia wakati akipatiwa matibabu.

“Ilipofika jioni muda wa saa moja mtoto aliomba chakula nikampatia akala badaye akasema mama sijashiba niongezee tena nikamuongezea chakula akala alipomaliza akanawa akatoka nje muda mfupi nikasikia mama nikakimbia kukuta fisi kamkamata nikamkimbiza alikuwa amemg’ata kwenye shingo nikaanza kupiga kelele akamuachia mtoto fisi alikimbia kidogo akaenda kusimama basi nikambeba mtoto majirani wakanisaidia kumkimbiza Hospital tumefika Hospital mtoto amefariki, naomba tu serikali itusaidie tutamaliza watuwekee ulinzi tutamaliza watoto kama kunasehemu wanajua wanapoishi wawawekee hata sumu wafe”

Baadhi ya wakazi wa kata ya kitangili Manispaa ya Shinyanga Wameiomba Serikali ngazi ya Wilaya na Mkoa kuchukua hatua za haraka kudhibiti fisi wanaoendelea kusababisha vifo na majeruhi hasa kwa Watoto wadogo.

Vifo vya watoto wadogo vitokanavyo na kushambuliwa na fisi vimeendelea kuchukua kasi katika mkoa wa Shinynga.