Mwalimu mkuu shule ya sekondari mzindakaya mkoani rukwa ajisalimisha polisi kwa kubaka


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim
Wangabo amewaagiza wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Rukwa
kuhakikisha Mkuu wa Shule ya Sekondari Mzindakaya iliyopo kata ya
Kaengesa, Wilayani Sumbawanga Dastan Mlelwa anafikishwa mahakamani
haraka iwezekanavyo baada ya kuwabaka na kuwatia mimba wanafunzi wawili
wa kidato cha pili na cha tatu katika shule hiyo.
Amesema kuwa anataarifa kuwa
mwalimu huyo tayari amekwishajisalimisha katika mikono ya polisi na
hivyo kumtaka kamanda wa polisi mkoa, Kamanda wa TAKUKURU mkoa pamoja na
Mkuu wa Usalama wa mkoa kufuatilia jambo hilo ili mwalimu huyo asitoke
kwenye mikono ya polisi bali apelekwe mahakamani.
“Hili jambo hatutalifumbia macho,
Mkuu wa shule kuwatafuta wanafunzi kimapenzi na mpaka kuwatia mimba,
yeye kama mzazi na mwalimu haikubaliki hata kidogo, huu ni ubakaji
kwasababu wale wanafunzi wa kidato cha pili na cha tatu hawana umri wa
miaka 18 ni chini ya hapo, ni ubakaji,” Alisisitiza.
Katika kusisitiza suala hilo pia
ameitaka kamati hiyo kufuatilia kesi ya Mwalimu wa Shule ya Sekondari
Mpui iliyoopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga aliyembaka na kumpa
mimba mwanafunzi wa kidato cha pili na baadaye mwanafunzi huyo
kuhamishwa katika shule ya Sekondari Mazwi iliyopo Manispaa ya
Sumbawanga.
Katika hatua nyingine Mh. Wangabo
amewaagiza wajumbe hao wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa kufuatilia
kesi ya wizi wa mifugo inayomhusisha Afisa mifugo wa mji mdogo wa laela,
wilayani Sumbawanga Emanuel Tluwey baada ya kukamatwa akiwa anachinja
ng’ombe wa wizi kesi ambayo ilifikishwa polisi na kuonya kuwa kesi hiyo
isifinyangwe finyangwe ili mwizi huoy asichukuliwe hatua.
“Lakini kuna Mazingira tata huenda
kesi ikafinyangwa finyangwa na mwizi huyu asichukuliwe hatua, sasa
narudisha kwa timu hii hapa, TAKUKURU yuko pale, jeshi la polisi na
vyombo vingine vya usalama fuatilieni suala hili kule Laela huyu mwizi
wa mifugo lazima achukuliwe hatua ya kisheria afikishwe mahakamani
haraka iwezekanavyo,” Alisema.


Mh. Wangabo ameyasema hayo wakati alipokuwa akiongea na
waandishi wa habari katika kikao maalum kilichowajumuisha wajumbe wa
kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na watumishi wa seksheni ya
Elimu na watumishi wa seksheni ya uchumi na uzalishaji inayojumuisha
watumishi wa mifugo katika Mkoa.
Mh. Wangabo amesema kuwa nia ya
kuyafanya hayo ni kupiga vita uhalifu ndani ya mkoa pamoja na ubakaji wa
wanafunzi na kuonya kuwa itafika wakati kutakuwa na kura za maoni
mashuleni kwa wanafunzi ili kumbaini anayewashawishi wanafunzi hao
kujiingiza katika suala la mapenzi katika umri mdogo.