Rwanda na uganda zakubaliana kubadilishana wafungwa

Serikali
za Uganda na Rwanda, Jumapili zilikubaliana kubadilishana wafungwa,
katika juhudi za kupunguza uhasama baina yao, baada ya kushutumiana kwa
mda mrefu na kufanyiana ujasusi unaotajwa na wachambuzi kama wenye lengo
la kutatiza amani ya kila upande.


Rais
wa Rwanda Paul Kagame, na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni ambao
walikuwa marafiki wakubwa sana kabla ya kutofautiana, walifikia
makubaliano hayo katika kikao cha mjini Luanda, Angola.

Viongozi
hao hao walisaini mkataba wa ushirikiano katika kurejesha hali ya
utulivu baina yao, mwezi Agosti mwaka uliopita, lakini utekelezaji wake
umekosa kasi ilivyiotarajiwa.

Japo
hakuna taarifa zaidi zimetolewa kuhusu makubaliano ya jumapili,
inafahamika kwamba viongozi hao wawili walikubaliana kubadilishana
wafungwa katika kikao kitakachofanyika Februari 21, kwenye mpaka
uliofungwa kati ya Rwanda na Uganda, mjini Katuna .

Kikao
cha Angola kilisimamiwa na rais Joao Lourenco, na kuhudhuriwa na rais
wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi.

Katika
taarifa ya kurasa mbili yenye vipengele 8 iliyotolewa na ikulu ya rais
wa Angola, viongozi hao waliahidi kushirikiana katika kuimarisha amani,
utulivu, ujirani mwema na kuaminiana.

“Pande
zote mbili zinatakiwa kujizuia na vitendo vinavyoweza kuleta hali ya
kutoaminiana au uhasama, kuhusiana na madai ya kufadhili makundi yenye
lengo la kutatiza serikali zake,” kinasema kipengele cha pili, aya ya
saba ya taarifa hiyo fupi.

Wiki
iliyopita, rais wa Rwanda Paul Kagame alisema kwamba hatashurutishwa
kufungua mpaka kati ya Rwanda na Uganda hadi serikali ya rais Yoweri
Museveni itakapotimiza matakwa ya serikali ya Rwanda ambayo ni pamoja na
kuachilia huru raia wake wote wanaozuiliwa katika magereza ya Uganda.

Rwanda ilifunga mpaka wake mwezi Februari mwaka uliopita na kupiga marufuku biashara kati yake na Uganda.

Hakuna
taarifa iliyotolewa iwapo Rwanda ipo tayari kufungua mpaka wa Katuna
ili kuruhusu raia wake kuingia Uganda, au Kuruhsu bidhaa za Uganda
kuingia Rwanda.

Rwanda inaishutumu Uganda kwa kufadhili makundi ya waasi yenye lengo la kupindua serikali ya rais Paul Kagame. 

-VOA