Serikali ya mapinduzi zanzibar yaimwagia sifa ucsaf

Na Mwandishi wetu, APC BLOG, ZANZIBAR


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) nchini kwa kuipa kipaumbele miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mfuko huo kwa upande wa Zanzibar.
 
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya alipotembelea Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) jijini Dodoma akiongozana na mwenyeji wake Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Atashasta Nditiye (Mb) pamoja na ujumbe wake kutoka katika Wizara anayoiongoza. 
Akizungumza na Uongozi wa Mfuko huo, alisema UCSAF imetoa kipaumbele kwa miradi mikubwa mitatu ambayo itaongeza maendeleo ya matumizi ya TEHAMA Visiwani Zanzibar.
“Nawashukuru sana kwa kujenga vituo vya mawasiliano Zanzibar na minara ya mawasiliano ambapo inawawezesha wananchi kutuia huduma za mawasiliano kwa shughuli za kijamii na kiuchumi visiwani humo. Aidha, ameongeza kuwa amefurahishwa  na mkakati wa kuwahamasisha wasichana kujitokeza na kupata mafunzo katika programu ya Wasichana na TEHAMA, “Hii itawafanya wasichana wa Zanzibar kuwa mstari wa mbele kutumia TEHAMA na kuingia katika mfumo wa Elimu ya TEHAMA,” amesema. 
Pia, ameishukuru na kuipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana  na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji katika kupanga na kutekeleza mipango mbali mbali inayohusu Sekta ya Mawasiliano kwa kuwa mawasiliano ni suala la Muungano. 
Naye Mhe. Nditiye (Mb) alisema kuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imefarijika sana kuupokea ujumbe wa Mheshimiwa Dk. Mamboya ambao umekuja Tanzania Bara kujifunza na kubadilishana uzoefu kuendana na utendaji kazi wa kila siku wa taasisi za Mawasiliano kwani mawasiliano ni suala la Muungano. 
Nditiye alimhakikishia Mhe. Dk. Mamboya kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itahakikisha inaendelea kutoa ushirikiano kwa SMZ kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji ili kuendelea kutekeleza majukumu na kuhudumia wananchi katika nyanja ya mawasiliano.
Wakati akitoa taarifa ya Wizara kwa ugeni huo, Nditiye alisema kuwa tayari Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imejenga na kufikisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo Unguja inaunganishwa na Mkongo huo kupitia mkongo wa baharini uliopo kwenye waya wa umeme kutoka Dar es Salaam na Pemba imeunganishwa kutoka Tanga. 
Pia, aliongeza kuwa vituo kumi vya TEHAMA vimejengwa na UCSAF kwa gharama ya shilingi milioni 754.8 ambapo vituo sita vimejengwa Unguja na vituo vine vimejengwa Pemba na tayari kila kituo kimepewa kompyuta saba na printa moja kutoka UCSAF
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya UCSAF aliishukuru Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji ya SMZ kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mfuko wakati wa kutekeleza miradi ya TEHAMA kwa upande wa Zanzibar. Alisema Wizara hiyo imekuwa karibu na Mfuko jambo ambalo limepelekea mafanikio ya miradi ya TEHAMA visiwani humo.
Akielezea utekelezaji wa miradi ya TEHAMA Visiwani Zanzibar, Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bibi Justina Mashiba amesema, jumla ya wasichana 40 kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamepewa mafunzo ya utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA kutoka mikoa ya Kaskazini Pemba na Mjini Magharibi. Aidha alisema Mfuko umetoa vifaa vya TEHAMA kwa shule 16 Zanzibar, uboreshaji wa mawasiliano kwenye Kata 10 zenye vijiji 18 Zanzibar.
Ujumbe wa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ukiongozwa na Mhe. Dkt Sira Ubwa Mamboya pamoja na kutembelea Ofisi za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, pia, ulitembelea mradi wa TEHAMA katika Shule ya ekondari ya Wasichana Msalato, Dodoma uliofadhiliwa na UCSAF na kutembelea mnara wa mawasiliano uliofadhiliwa na UCSAF uliopo Dodoma, Wilayani Bahi kijiji cha Makanda. Pia, ujumbe huo utaendelea na ziara yake kwa kutembelea taasisi mbalimbali za Mawasiliano za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Tanzania Bara.

Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano