Na Seif Mangwangi, Arusha
Serikali imesema itaendelea na zoezi la kuondoa makundi mbalimbali ya watu na mifugo yaliyovamia maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo kwenye maeneo ya misitu na hifadhi za Taifa.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa bodi ya ushauri ya wakala wa misitu nchini, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt Pindi Chana amesema zoezi lililofanywa hivi karibuni wilaya ya Mbarari katika hifadhi ya Ihefu kuondoa mifugo iliyovamia hifadhi hiyo ni endelevu na kuwataka wafugaji kokote walipovamia maeneo ya hifadhi waanze kuondoka.
” Nawatumia salamu watu wote waliovamia maeneo ya hifadhi, kile kilichofanyika Ihefu tunakuja na maeneo mengine, tunafanya hivi ili kuhakikisha tunaokoa mazingira yetu ambayo yako hatarini kutokana na kuvamiwa sana,”anasema.
Dk Pindi Chana amesema kwa sasa Wizara, kwa kushirikia na mamlaka nyingine, inaendelea kutekeleza maamuzi ya Kamati ya Mawaziri nane iliyoundwa kwa ajili ya kutatua migogoro inayokabili maeneo ya hifadhi kwa kupitia maeneo ya misitu yaliyovamiwa na kuanzishwa vijiji au makazi.
Amesema maamuzi hayo mara nyingi yamejikita aidha kurasimisha maeneo yaliyovamiwa, kuyahamisha au kufuta baadhi ya maeneo hayo na kwamba maamuzi hayo yanalenga kuondoa changamoto iliyokuwepo ya maeneo mengi kuwa na shughuli za kibinadamu zinazosababisha uharibifu mkubwa wa misitu.
“Baada ya mapitio hayo, maeneo yote yatakayobaki kama hifadhi yatapaswa kusimamiwa kikamilifu na kuondoa kabisa uwezekano wa uvamizi na uharibifu. Bodi hii itapaswa kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi endelevu na unaozingatia sheria kwa maeneo yote ya misitu inayosimamiwa na Serikali Kuu,” amesema.
Aidha ameitaka bodi hiyo kubuni mikakati itakayowezesha mashamba ya miti kuongezeka na kusimamiwa kwa njia endelevu na kukuza na kuendeleza utalii kwenye hifadhi za misitu ya mazingira asilia na kuwa na mikakati thabiti ya kukuza uchumi wa viwanda kwa kupitia utendaji wa Wakala na ushirikiano na Sekta binafsi au Wananchi na hivyo kutekeleza dhana ya mahusiano ya kibiashara baina ya Serikali na Sekta binafsi.
Akitoa neno la shukurani kwa waziri, Mwenyekiti wa bodi hiyo brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremi amesema yeye na bodi yake watahakikisha wanatekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri ikiwa kuongeza mapato na gawio kwa Serikali.
Bodi hiyo yenye wajumbe sita inaongozwa na Mwenyekiti Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremi, wajumbe ni wakili Pensia Kiure, Mhandisi Enock Nyanda, Dkt Siima Makegesa, Bahati Masila na Profesa Do santos Silayo ambaye ndio Mkurugenzi mkuu wa wakala wa Misitu.