Baadhi ya waandishi wa habari na watumishi wa Wizara wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama,(hayupo pichani) |
Na Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama,ametangaza ajira mpya zaidi ya 32,000 katika sekta za ualimu,afya,kilimo,mifugo,uvuvi na maji huku watumishi 92,000 wakipandishwa vyeo na 6026 wakibadilishiwa kada.
Katika sekta ya ualimu imetoa ajira 12,035 ambapo nafasi 9,800 kwa ajili ya walimu wa shule za msingi na sekondari,afya nafasi 10,285 zinazojumuisha nafasi 7,612 kwa ajili ya Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati zilizopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Hayo yameelezwa leo Aprili 12,2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Jenista Mhagama wakati akitoa kuhusu utoaji wa vibali vya ajira kwa watumishi wa umma nchini.
Waziri Mhagama amesema Serikali imeamua kutekeleza ahadi yake ya kuajiri watumishi wengine 32,604 kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha na mchakato wa ajira hizi unaanza leo.
“Niseme tu Taarifa hii ni hatua ya kwanza ya mchakato wa kuhakikisha utekelezaji wa ajira hizo unakamilika kabla ya mwaka wa fedha 2021/22 haujaisha. Utekelezaji wa Ajira hizi utaigharimu Serikali kiasi cha shilingi 26,297,541,175.00 kwa mwezi sawa na Shilingi 315, 570,494,100.00 kwa mwaka,”amesema.
Waziri Mhagama ameongeza kuwa katika ajira hizo mpya Serikali imezingatia mgawanyo wa ajira katika Sekta mbalimbali zikiwemo Elimu,Afya,Kilimo, Maji, Mifugo, Uvuvi pamoja na maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa wa watumishi.
Aidha Waziri Mhagama ameziagiza Mamlaka za Ajira, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Afya pamoja na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuhakikisha wanaendesha michakato ya ajira kwa uwazi, weledi, uadilifu.
“Pamoja na kutoa fursa sawa kwa waombaji wote kuweza kushiriki katika mchakato wa ajira hizi ili Serikali iweze kupata watumishi mahiri na wenye sifa stahiki,”amesema.
Amesema sekta ya kipaumbele ni elimu ambayo imetengewa jumla ya nafasi 12,035 ambapo nafasi 9,800 kwa ajili ya walimu wa shule za msingi na sekondari.
Amesema mchakato wa ajira hizo utasimamiwa na Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Amesema nafasi 2, 235 ni kwa ajili ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya juu pamoja Wakufunzi wa Vyuo vilivyopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Waziri huyo amesema mchakato wa ajira hizo utasimamiwa na Taasisi husika za elimu kwa kushirikiana na Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma.
Amesema sekta ya Afya imekasimiwa nafasi za ajira 10,285 zinazojumuisha nafasi 7,612 kwa ajili ya Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati zilizopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Amesema mchakato wa ajira hizo utasimamiwa na Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Amesema nafasi zingine 1650 kwa ajili ya kuajiri watumishi wa kada za Afya katika Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Wizara ya Afya huku Nafasi 1023 kwa ajili ya Vyuo vya Afya.
“Hospitali nyingine za kimkakati na zile za Mashirika ya Dini (District Designated Hospitals-DDHs) na Hiari ( Voluntary Agency-VAHs) zenye mkataba na Serikali ambapo Mchakato wa ajira hizo utasimamiwa na Wizara ya Afya kwa Vyuo vya Afya na Hospitali nyingine za kimkakati na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kwa Hospitali za DDHs na VAHs,”amesema.
Amesema nafasi 2,392 zinatarajiwa kujazwa kwenye sekta zingine za kipaumbele ikiwa ni pamoja na kada za Kilimo nafasi za ajira 814,Kada za Mifugo nafasi 700,Kada za Uvuvi nafasi 204,Kada za Maji nafasi 261 na Kada za Sheria nafasi 513.
Amesema mchakato wa ajira hizo utasimamiwa na Wizara pamoja na Sekretarieti ya ajira katika Utumishi wa Umma.
Amesema nafasi zingine 7,792 kwa ajili ya kuajiri Watumishi wa kada nyingine kwenye Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine za Umma.
Amesema mchakato wa ajira hizi utasimamiwa na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine za Umma pamoja na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
“Nichukue fursa hii kuwaasa waajiri na waombaji wa ajira mpya kujiepusha na vitendo vya rushwa na udanganyifu hususan wa vyeti vya elimu na taaluma wakati na baada ya mchakato wa ajira hizi.
“Nitumie fursa hii kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) kufuatilia kwa karibu mchakato mzima wa ajira hizi ili kuweza kubaini na hatimaye kuzuia mianya yote ya rushwa na upendeleo,”amesema.