Korea kaskazini yaitaka marekani kubadili mwelekeo wa mazungumzo ya nyuklia

Wakati
muda wa mwisho wa mazungumzo na Marekani juu ya mpango wa nyuklia wa
Korea Kaskazini ukiwadia, kiongozi wa taifa hilo, Kim Jong Un, ameitisha
mkutano wa dharura wa maafisa wakuu wa kijeshi na kidiplomasia.


Kwenye taarifa yake ya leo, shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini
(KCNA) limesema kiongozi huyo alizungumza kwenye mkutano maalum wa Chama
cha Wafanyakazi wa Korea, akielezea matatizo yanayoikumba sekta ya
viwanda na wakati huo huo akiwapangia majukumu wasaidizi wake
kurekebisha matatizo hayo.

Kim alitaka pawepo na matayarisho ya haraka ya kisera juu ya masuala ya
kiusalama, silaha na kile alichosema kuwa ni ulinzi wa uhuru wa Korea
Kaskazini.

Kauli hizi zimetafsiriwa na mahasimu wake wa Korea Kusini na Marekani
kwamba ni dalili zisizo njema kuelekea muda wa mwisho aliokuwa ameuweka
wa tarehe 31 Disemba 2019, ambapo alitaka utawala wa Rais Donald Trump
wa Marekani uwe umeshalainisha msimamo wake kwenye mazungumzo ya mpango
wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Kuna wasiwasi kwamba huenda kwenye hotuba yake ya mkesha wa mwaka mpya,
Kim akaamuru kusitishwa kwa mazungumzo hayo na badala yake kurejea
kwenye majaribio ya makombora ya masafa marefu, ambayo aliyasitisha
tangu mwaka 2017.

Korea Kaskazini inaitaka Marekani kuacha kuiwekea vikwazo mara moja, ikiwa inataka kuyaokowa mazugumzo  hayo.

Credit:DW