Shirika la posta lazikutanisha taasisi za serikali kufanya kazi katika ofisi moja

 

Kaimu Postamasta Mkuu Macrice Mbodo
akieleza jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia
Zainab Chaula alipotembelea ofisi za Shirika la Posta na kuangalia namna
walivyojiandaa kwa ajili ya huduma ya One stop Centre (Huduma Pamoja
Centre) itakayotoa huduma taasisi zote za Kiserikali nchi nzima.

Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na
Teknlojia Zainab Chaula akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wakuu
wa Taasisi mbalimbali wa Kiserikali watakaokuwa wanatoa huduma zao ndani
ya ofisi za Shirika La Posta Nchini.

………………………………………………………

Na.Mwandishi wetu

SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC)
limeanza kutoa Huduma Pamoja Centre kwa taasisi za kiserikali ili
kurahisha na kupunguza usumbufu kwa wananchi.

Huduma hiyo iliyoanza kutolewa Julai Mosi mwaka huu inazihusisha
taasisi zote za kiserikali za zitatoa huduma zote ndani ya ofisi moja.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia
Zainab Chaula amesema mpango huo ni mkakati wa muda mrefu wa serikali
katika kuziunganisha taasisi za kiserikali kufanya kazi kwenye ofisi
moja.

 

Akizungumza na waandish wa habari baada ya kutembelea
ofisi za Shirika la Posta Jijini Dar es Salaam, Chaula amesema serikali
inaendelea kutekeleza miradi yake kidigitali kwa kuzileta taasisi zote
muhimu pamoja ndani ya ofisi moja ambayo nayo ni Shirika la Posta.

 

Amesema Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia imeweka mikakati katika
kusimamia mifumo ya kidigitali ili kupunguza usumbufu kwa wananchi pindi
wanapotaka huduma kwa uharaka zaidi.

Chaula amesema amefanya kikao na wakuu wa taasisi zote na kuwataka
waongeze muda wa kufanya kazi ili wananchi wengi waweze kupata huduma.
 

 Huduma
hizo zote zitakuwa zinatolewa ndani ofisi za Posta ambapo kwa sasa
imeanza katika mkoa wa Dodoma na Dar es salaam na amezipongeza taasisi
zote kwa kuweza kuamua kwa pamoja kuweka ofisi za Posta kwasababu kila
siku wanataka huduma na njia rahisi ni kuwasogezea karibu

Kaimu Postamasta Mkuu Macrice Mbodo amesema hadi kufikia Septemba
mwaka huu watakuwa wamefikia ofisi 10 zitakazokuwa zinatoa huduma hizo.

 

Amesema Shirika la Posta lipo nchi nzima na huduma
hizo zitakuwa zinapatikana ndani ya ofisi zao zote na kwa hilo itaondoa
usumbufu na gharama kwa wananchi. 

Amesema shirika wamejipanga kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi wote

Kaimu Mtendaji Mkuu Mamlaka ya Usajili Vizazi na Vifo RITA Emmy
Hudson amesema katika ofisi za Posta watakuwa wanatoa huduma ya vyeti
vya kuzaliwa na vifo. 

Amesema kwa sasa ukifika katika
ofisi za Posta ndani ya Jiji la Dodoma na Dar es salaam utakuta ofisi
zao na huduma zote utazipata na itapunguza usumbufu kwenda ofisi za
RITA.

Ameishukuru na kuipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa wananchi kupata huduma zote muhimu ndani ya ofisi moja.

 

Kwa sasa ndani ya ofisi za shirika la posta litakua linatoa huduma
mbalimbali za kitaasisi kama NIDA, BRELA, RITA, NSSF, uhamiaji na
zinginezo.