Sida na harakati zake za kunusuru waandishi wa habari dhidi ya ugonjwa wa corona

 

Na Mustafa 
Leu. 

ULIMWENGU upo katika
taharuki  kubwa inayotokana na kukumbwa na ugonjwa wa mlipuko wa Covid-19
ambao mpaka sasa hauna tiba wala kinga na umesababisha  maelfu ya watu
kufariki dunia .

Wataalam wa afya
wanaendelea kukesha kwenye maabara kutafuta dawa na tiba sahihi ya ugonjwa huu
wa Covid-19 ambao haujafahamika chanzo chake mbali ya kuwa na madhara makubwa
ikiwemo vifo na kuporopmoka kwa uchumi.

Baada ya kulipuka kwa
ugonjwa huo kila nchi imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana nao kwa lengo
la kuutokomeza na kuwakinga wananchi wake wasipate maambukizi na kuathiri
uzalishaji.

Miongoni mwa hatua za
awali zilizochukuliwa hapa nchini kwetu ni pamoja na Serikali kushauri viongozi
wa dini kuhakikisha wanaendesha ibada maalumu kwa waumini wake kwa kumuomba Mungu
kutuepusha na janga hilo, hamasa ambayo iliwashirikisha hadi viongozi wa
mila.

Tuna kila sababu ya
kumshukuru mungu, kwa kutunusuru na maambukizi hayo ya ugonjwa huo wa Covid-19
na sasa tupo salama,lakini wakati sie tupo salama zipo nchi zinazotuzunguka
bado zina kabiliwa na tatizo hilo kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa
huo.

Ongezeko hilo la
maambukizi linazifanya nchi hizo kukuna vichwa ni namna gani wataepukana na
maambukizi kwa kuwa kila siku taarifa zinaonyesha kwamba kiwango cha maambukizi
bado kinaongezeka hivyo nchi hizo zinaendelea kuchukua hatua kwa kuweka masharti
kwa wananchi wake ili waweze kujikinga na maambukizi .

Afisa Programu wa UTPC Victor Maleko akizungumza na wanachama wa Arusha Press Club wakati wa mafunzo kuhusu magonjwa ya mlipuko yaliyofanyika hivi karibuni Arusha, wa pili kulia kwake ni Claud Gwandu Mwenyekiti wa APC na wa kwanza kushoto kwake ni Mussa Juma Makamu Mwenyekiti wa APC

.Wanachama wa klabu ya waandishi wa habari Arusha wakimsikiliza kwa makini mwezeshaji wa mafunzo kuhusu magonjwa ya kuambukiza Dkt Francis David (hayupo pichani), mafunzo hayo yalidhaminiwa na UTPC.

Mbali na Viongozi wa
dini kuendesha Ibada maalumu, pia serikali ilihamasisha matumizi ya dawa za
asili zikiwemo za kujifukiza, kuhamasisha matumizi ya viungo mbalimbali kama
tangawizi, limao, na ulaji wa matunda kwa wingi .

Pia ilitolewa hamasa
kwa wananchi kusikiliza ushauri wa wataalamu wa afya kuhusu hatua za kujikinga
na maambukizi hayo ya ugonjwa huo wa Covid -19.

Pia kulitengwa maeneo
maalumu ya kuhudumia watu watakaokuwa wamepata maambukizi ya ugonjwa huo ili
wasiusambaze na kuenea kwa watu wengi zaidi.

Katika kuhakikisha
ugonjwa huo hauenei ,Ulimwengu ulisitisha safari zote zikiwemo za ndege,meli,
treni,magari,kutoka nchi moja kwenda nyingine,kuweka vizuizi au karantini
wagonjwa wa Covid-19.

Wakati wa kutekeleza
hatua hizo uchumi ulimwenguni umeporomoka ambapo shughuli za uzalishaji wa
 bidhaa ikiwemo utalii  zilishuka kwa kiwango kikubwa sana na hata
kupunguzwa kwa wafanyakazi kwenye maeneo mbalimbali .

Kutokana na ulimwengu
kukumbwa na maambukizi hayo Shirika la misaada la Sweden, SIDA, linajitokeza
kuendesha mafunzo ya kuwakinga wanahabari dhidi ya  maambukizi hayo ya
ugonjwa huo wa Covid-19.

Lengo la mafunzo hayo
ni kuwawawezesha wanahabari kujikinga na kuwa na tahadhari dhidi ya 
kupata maambukizi hayo kutokana na wao kuwa ni miongoni mwa jamii inayoweza
kuambukizwa kwa haraka kutokana na kufanya kazi kwenye mazingira hatarishi.

Sida, imefadhili
 mafunzo hayo kupitia mradi wake unaosimamiwa na Umoja wa vilabu vya
wanahabari nchini UTPC, ili kuwaokoa wanahabari wasiambukizwe ugonjwa huo ambao
hauna kinga wala tiba.

Mafunzo hayo
yanatolewa kutokana na kutambua umuhimu mkubwa wa wanahabari kuwa ni kundi
ambalo lipo katika hatari kubwa ya kukumbwa na ugonjwa huo.

 Pia Wanahabari
ni kundi muhimu katika maendeleo ya nchi kutokana na unyeti wa kazi zao wanazozifanya
za kuelimisha na kuhabarisha umma.

Kutokana na wanahabari
kuwa kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi hayo kutokana na kufanya kazi
kwenye mazingira hatarishi Shirika hilo la Sida,likaona ni muhimu kutoa mafunzo
ya kuwakinga wanahabari nchini dhidi ya  maambukizi ya ugonjwa huo wa
mlipuko wa Covid -19.

Katika kuhakikisha
wanahabari wanapewa dozi ya mafunzo ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo UTPC
ilitoa mwongozo kuwa klabu za waandishi wa habari kutafuta wataalamu wa afya
kutoa mafunzo hayo kwa wanahabari kutokana na uzoefu wao wa namna ya kujikinga
dhidi ya magonjwa ya mlipuko .

Mafunzo hayo
yanajikita kuwaokoa wanahabari ili wasipate maambukizi ya ugonjwa huo,na hivyo
kuwawezesha kuendelea na majukumu yao wakiwa salama.

Hongera sana SIDA,kwa
kuliona hilo la umuhimu wa mafunzo kwa wanahabari kwa kuwa wanahabari
wakiambukizwa ugonjwa huo wa mlipuko umma utakosa taarifa na hivyo nchi
itaangamia.

Kwa kipindi kirefu
SIDA imekuwa ni nguzo na muhimili mkubwa wa sekta ya habari nchini imekuwa
ikifadhili mafunzo mbalimbali kwa lengo la kuwanoa kwenye taaluma ili wawe ni
mahiri .

Afisa Programu wa
UTPC,Victor Maleko akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo anasema kuwa
mafunzo hayo yanayoambatana na kutolewa vifaa vya kujikinga yanawezesha
wanahabari kuepuka maambukizi.

Anasema mafunzo hayo
ni muhimu sana kuliko kitu kingine chochote kwa mwanahabari kwa kuwa wao ndio
tegemeo la wananchi kupata taarifa za maambukizi na hatua za kujikinga.

Kwa upande wake
Daktari Francis David, kutoka hospitali ya Aghakhan tawi la Arusha ,akiendesha
mafunzo hayo anasema kuwa  ni muhimu kwa wanahabari kupewa elimu hiyo
kutokana na umuhimu wao kwa kuwa umma.

Anasema
Umma,unawategemea wanahabari  kupata taarifa kuhusu kiwango cha maambukizi
na hatua za kuchukua kujikinga na maambukizi hayo ya ugonjwa huo wa mlipuko.

Anasema kirusi hicho
cha Covid-19 kina weza kuishi kwenye sehemu yeyote kwa muda wa saa 8 kutoka kwa
mtu aliyeambukizwa mara baada ya kupiga chafya kwa kuwa kinakuwa bado kipo
kwenye mazingira ya majimaji.

Kirusi hicho ambacho
huambukiza  kwa njia ya hewa ,kugusa maeneo ya wazi ambayo ni pua,macho na
mdomo ambapo kirusi kikishaingia mwilini na kukaa kwenye koo na kisha kuingia
ndani ya mwili .

Anasema kikisha kaa
ndani ya mwili  hukaa kwenye mapafu na kusababisha mzunguko wa damu
kuganda na hatimae kifo.

Kabla ya kifo kirusi
hicho  huwa kinasababisha homa kali ya mapafu, ambayo husababisha 
mafua makali, mtu kushindwa kupumua  na kuhema .

Waathirika wakubwa wa
ugonjwa huo wa mlipuko ni wazee ambao tayari miili yao imepungukiwa na kinga ya
mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali yatakayowashambulia ikiwemo ya mlipuko.