Siku ya uchaguzi yawekwa wazi zanzibar.


TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) leo imetangaza rasmi tarehe ya siku ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar kuwa utafayika siku ya jumatano ya Oktoba 28 mwaka huu.

 

Pia Tume imesema  imeamua kutangaza tarehe hiyo ya kupiga kura kufuatia kutamkwa kwa tarehe rasmi ya kuvunjwa kwa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ambayo ni Agasti 20 mwaka huu.

 

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kutangaza kwa tarehe hiyo, katika ofisi za Tume hiyo Maisara Mjini Unguja.

 

Alisema, kuvunjwa kwa Baraza la Wawakilishi kunatoa nafasi kwa Tume kuanza mchakato utakaowezesha kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa kumchagua Rais, wajumbe wa baraza la wawakilishi na Mdiwani.

 

“Kama nilivyosema katika maelezo yangu hapo juu kuwa, Baraza la wawakilishi litavunjwa rasmi Agasti 20 mwaka huu, hivyo ZEC kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 34 (3) na (4) cha sheria ya uchaguzi nambari 4 ya mwaka 2018, inatangaza rasmi kuwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar utafanyika Octoba 28 mwaka huu,” alisema.

 

Aidha alisema sheria ya uchaguzi imetoa nafasi ya kufanyika kwa kura ya mapema hivyo alisema upigwaji wa kura hiyo ya mapema utafanyika Oktoba 27 mwaka huu siku moja kabla ya upigaji wa kura wa pamoja.

 

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar alieleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 82 cha sheria ya uchaguzi nambari 4 ya mwaka 2018, kinasema upigaji kura ya mapema utawahusisha watendaji wanaosimamia majukumu ya siku ya uchaguzi.

 

Akiwataja watendaji hao alisema ni pamoja na wasimamizi wa uchaguzi, wasaidizi wa uchaguzi, wasimamizi wa vituo, askari polisiwatakaokuwa kazini siku ya uchaguzi, wajumbe wa tume ya uchaguzi pamoja na watendaji wa tume na wapiga kura ambao watahusika na kazi ya ulinzi na usalama.