Tanzia: diwani kata ya mwamalili afariki dunia

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Aliyekuwa Diwani wa kata ya Mwamalili katika Manispaa ya Shinyanga Paul  Machela amefariki dunia jana katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga alipokuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu.

Akitoa taarifa juu ya kifo hicho katibu wa itikadi, Siasa na uenezi wa chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Said Bwanga amesema diwani Machela amefariki jana majira ya saa kumi na mbili Asubuhi na kwamba chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini  kwa kushirikiana na familia ya marehemu wanaendelea  kuandaa taratibu za mazishi.

Akimwelezea diwani huyo Bwanga amesema chama cha Mapinduzi pamoja na wananchi wa kata ya Mwamalili watamkumbuka kiongozi huyo kutokana na utendaji kazi wake wenye uadilifu na uzalendo ambapo amewataka wananchi wa kata hiyo kuwa wastahimilifu kutokana na msiba huo.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Mheshimiwa Elias Masumbuko amesema  mazishi yatafanyika kesho katika kijiji na kata ya Mwalili  Manispaa ya Shinyanga ambayo  yatatanguliwa na ibada kwa imani ya kanisa katoliki.

Mstahiki Meya amesema kifo cha Mheshimiwa Machela kimeacha pengo kubwa katika kata yake ya Mwamalili,Chama chake cha Mapinduzi-CCM,pamoja na halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga  kutokana na utumishi wake uliotukuka katika kipindi chote ambacho amekuwa kiongozi kwa nafasi mbalimbali.

“Alichaguliwa na wananchi wa eneo lake kuwa Barozi wa eneo hilo toka Mwaka 1988 mpaka 1992 akiwa kwenye wigo huo huo wa kisiasa alifanikiwa kupata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa kitongoji  katika eneo hilo toka Mwaka 1996 mpka 1998 na bado katika wigo huo huo wa kisiasa alifanikiwa kupata nafasi ya kuwa mwakirishi wa eneo hilo kwa nafasi ya udiwani kutoka Mwaka 2000 mpaka Mwaka 2021 ambayo mauti yamempata kwa maana ya kwamba nafasi hiyo ameitumikia kwa muda wa Miaka 21 mpaka siku ya mauti yake”.

Marehemu Paulo Machela alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifua kikuu pamoja na moyo kupanuka na kwamba ameacha Watoto 14 kati yao saba ni watoto wa kike.

Marehemu Paulo Machella alizaliwa mnamo Disemba 20,Mwaka 1950 ambapo alisoma mpaka darasa la Nane na kwamba tofauti na masuala ya kisiasa alikuwa akijihusisha pia na shughuli za kilimo na ufugaji.

Paulo Machela alianza safari yake katika medani za Siasa alipochaguliwa na wananchi katika eneo lake, kuwa Balozi wa Chama hicho ngazi ya Shina mnamo Mwaka 1988 hadi 1992,na baadaye Mwaka 1996 hadi 1998 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwamalili,ambapo Mwaka 2000 alichaguliwa kuwa diwani wa kata ya Mwamalili nafasi ambayo ameitumikia kwa Miaka 21 mpaka mauti yalipomfika.