Trump atangaza kuuawa kwa kiongozi wa is abu bakr al-baghdadi syria



Rais
wa Marekani Donald Trump amethibitisha kuwa vikosi maalum vya Marekani
vimemuua kiongozi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS Abu Bakr
al-Baghdadi kaskazini mwa Syria.


“Jana usiku, Marekani ilifikisha mwisho safari ya gaidi nambari moja duniani,” alisema Trump. “Al-Baghdadi amefariki dunia”


“Alifika mwisho wa handaki wakati mbwa wetu wakimfukuza,” Aliongeza
Trump. Al-Baghdadi aliripua mabomu aliyokuwa amejifunga mwilini wakati
wanajeshi walipomkaribia. Mlipuko huo uliwauwa wanawe watatu.
Vikosi maalum vya Marekani viliweza kumtambua Baghdadi dakika 15 baada
ya kuuawa kwa kufanya vipimo vya vinasaba – DNA katika eneo la
shambulizi hilo. Uchunguzi huo wa DNA ulikuwa muhimu ikizingatiwa kuwa
al-Baghdadi alikuwa ametangazwa kuuawa mara kadhaa. Hakukuwa na hasara
yoyote kwa upande wa Marekani wakati wa operesheni hiyo.
Trump amesema katika Ikulu ya White House kuwa “idadi kubwa ya
wapiganaji wa al-Baghdadi na marafiki waliuawa, wakati watoto 11 wadogo
wakihamishwa kutoka kwenye nyumba walimokuwa, bila kujeruhiwa.
Amesema dunia sasa ni mahala salama, na kuwa “matukio hayo ni ukumbusho
mwingine kuwa tutaendelea kuwawinda magaidi waliobaki wa IS hadi
mwisho.”
Trump ameipongeza Urusi, Uturuki, Syria na Iraq klwa ushirikiano wao.
Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imesema katika taarifa kuwa Uturuki na
Marekani zilibadilishana taarifa kuhusu shambulizi hilo lililoongozwa na
Marekani mkoani Idlib, Syria. Kamanda wa vikosi vya Syrian Democratic –
SDF, Mazloum Abdi ameandika kwenye Twitter kuwa kifo cha al-Baghdadi
kilikuwa matokeo ya ushirikiano wao na Marekani.
Kwa miezi mitano kumekuwa na ushirikiano wa pamoja wa taarifa za
kijasusi na uchunguzi mahsusi, hadi tulipofanikisha operesheni ya pamoja
ya kumuua Abu Bakr al-Baghdadi,” Aliandika Abdi.
Al-Baghdadi amekuwa mafichoni mwa miaka mitano. Kuna wakati Marekani
ilitangaza zawadi ya dola milioni 25 kwa yeyote ambaye alikuwa na
taarifa ambazo zingesaidia kupatikana kwake.


Credit;DW