Tume ya haki za binaadam na utawala bora kuandaa mpango mkakati wa biashara na haki za binaadam, lengo ni kuepusha migogoro ya mara kwa mara inayotokea maeneo ya biashara

Na Seif Mangwangi, Arusha 

 TUME ya Haki za binaadam na Utawala bora nchini, iko kwenye mchakato wa kutayarisha mpango mkakati wa Kitaifa wa utekelezaji, usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za biashara na haki za binaadam (Business and Human rights activities) ili kuhakikisha haki za binaadam zinafuatwa katika maeneo ya kazi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uchunguzi ya ana kwa ana kwa maafisa wa tume hiyo mara baada ya kumaliza mafunzo yaliyokuwa yakiendeshwa kwa njia ya mtandao, Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Patience Ntwina amesema tume yake imepewa jukumu la kuandaa mpango huo na wizara ya katiba na sheria. 
 Amesema kazi ya kuandaa mpango mkakati huo utaanza hivi karibuni mara baada ya bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba kupangwa na kwamba wadau mbalimbali watashirikishwa katika kutoa maoni yao. 
 “Wizara ya Katiba na Sheria imeona tume yetu inaouweza wa kutengeneza mpango mkakati huo, na wadau wote watahusishwa ili kuhakikisha mpango huu unakuwa suluhisho la matatizo ya uvunjifu wa haki za binaadam maeneo ya biashara,”amesema.
 Amesema mafunzo yanayoendeshwa na tume hiyo kwa ushirikiano na wataalam wa haki za binaadam kutoka shirika la maendeleo la Denmark (DANISH), yanawajengea uwezo maafisa wa tume hiyo kwenye masuala ya utafiti na uchunguzi ili kuwarahishishia katika utendaji wao wa kazi.
 “Katika hotuba yangu ya ufunguzi nimewasisitiza wafanyakazi wenzangu wawe makini kusikiliza kile wanachofundishwa, hii itasaidia tume yetu kwenye ufuatiliaji na uchunguzi wa matukio ya haki za binaadam hasa maeneo ya biashara na haki za binaadam,”amesema.
 Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi idara ya malalamiko na Uchunguzi katika tume hiyo, Susan Pascal amesema mafunzo yanayotolewa yatakuwa muarobaini wa utatuzi wa migogoro inayotokea katika maeneo ya biashara na kazi. 
 Amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kutokana na ongezeko kubwa la muingiliano wa wananchi katika maeneo ya kazi na kumepelekea ongezeko la malalamiko ya uvunjaji wa haki za binaadam, hivyo mafunzo hayo yatawawezesha kupata mbinu zaidi ya kufanya uchunguzi na kutatua migogoro hiyo.
Katibu Mkuu Mtendaji wa Tume ya Haki za binaadam na Utawala bora, Patience Ntwana akisoma hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya ana kwa ana kati ya maafisa uchunguzi wa tume hiyo na wakufunzi kutoka shirika la maendeleo la Denmark Danish 
Maafisa uchunguzi wa tume ya haki za binaadam na utawala bora wakisikiliza hotuba ya ufunguzi
Maafisa uchunguzi wa kutoka tume ya haki za binaadam na utawala bora wakifuatilia hotuba ya ufunguzi 
Maofisa uchunguzi wakifuatili hotuba ya mgeni rasmi 
Maafisa uchunguzi kutoka tume ya Haki za binaadam na Utawala bora  pamoja na wakufunzi wakiwa katika picha ya pamoja