Ujenzi wa majengo ya utawala kuongeza tija utoaji huduma tamisemi

Na Ismail Ngayonga, MAELEZO

UTAWALA
bora ni nyenzo muhimu katika kuharakisha maendeleo endelevu ya nchi kwa
kuzingatia misingi ya sheria, uwazi na uwajibikaji ili kutoa huduma
bora kwa wananchi.

Ofisi
ya Rais-TAMISEMI inasimamia utekelezaji wa shughuli za utawala bora kwa
kuzingatia matakwa ya  Ibara  ya  146(1)  ya  Katiba  ya  Jamhuri  ya 
Muungano  wa  Tanzania  ya  mwaka  1977 inayohusu ugatuaji wa madaraka
kwa wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo.

Katika
Mwaka wa Fedha 2018/2019, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeendelea kuimarisha
utawala bora ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo ya utawala katika
Mikoa, Halmashauri, Tarafa, Kata, Mitaa na Vijiji ili kuboresha
mazingira ya kufanyia kazi.

Aidha
ili kufikia malengo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wake, Serikali
imeendelea kuwajengea uwezo viongozi na Watendaji kwenye Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuimarisha misingi ya uwazi, uwajibikaji
na usawa katika matumizi ya fedha kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Tangu
mwaka 1984, Serikali iliporejesha Mfumo wa Serikali za Mitaa, jitihada
kubwa zimekuwa zikifanyika katika kujenga mfumo imara wa kitaasisi ili
kusimamia na kuratibu shughuli za utawala, utendaji na maendeleo katika
ngazi ya Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Tarafa, Kata, Kijiji, Mtaa na
Kitongoji.

Agenda
ya kuziimarisha Serikali za Mitaa iliyoidhinishwa mwaka 1996, ina lengo
la kukidhi mahitaji ya kuwawezesha wananchi kushiriki kwa ukamilifu
katika shughuli za maendeleo na kutanzua changamoto kadhaa zilizozikumba
Serikali za Mitaa kwa muda mrefu.

Akiwasilisha
Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka
2019/2020, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo anasema Ofisi ya  Rais-TAMISEMI 
imeendelea kutimiza jukumu  la  msingi  la  kuzijengea uwezo Tawala za
Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi.

Anasema
katika katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, Tawala za Mikoa zimetumia jumla
ya shilingi bilioni 31.64 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa Ofisi na
nyumba za viongozi katika Mkoa, Wilaya na Tarafa.

‘Kati
ya Fedha hizo, shilingi bilioni 20.6 zimetumika kwa ajili ya ukarabati
na ujenzi wa Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Tarafa na
shilingi bilioni 11.04 zimetumika kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa
nyumba za viongozi kwenye Mikoa, Wilaya na Tarafa’’ anasema Waziri Jafo.

Waziri
Jafo anasema ujenzi na ukarabati wa Ofisi za Wakuu wa Mikoa umefanyika
katika Mikoa ya Katavi, Simiyu, Njombe, Geita, Pwani, Arusha, Ruvuma,
Dodoma na Singida kwa gharama ya shilingi bilioni 7.2 na pia ujenzi na
ukarabati wa Ofisi za Wakuu wa Wilaya umefanyika katika Wilaya 29
sambamba na kujenga ofisi 60 za za Maafisa Tarafa kwa gharama ya Tsh.
Bilioni bilioni 3.3.

Kwa
mujibu wa Waziri Jafo anasema katika mwaka 2018/19, Serikali imejenga
nyumba za viongozi 72 katika Mikoa na Wilaya kwa ajili ya Wakuu wa
Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa,
Makatibu Tawala wa Wilaya na Maafisa Tarafa, ambapo hadi kufikia mwezi
Februari 2019 ujenzi na ukarabati wa nyumba hizo umegharimu jumla ya
shilingi bilioni 11.04.

Akifafanua
zaidi Waziri Jafo anasema Halmashauri 78 zimeendelea na ujenzi wa
majengo ya utawala zikiwemo Halmashauri 55 zilizotengewa bajeti ya
shilingi bilioni 61.7 kuanzia mwaka wa Fedha 2015/16 hadi 2017/18,
ambapo ujenzi wa majengo hayo upo katika hatua mbalimbali za
ukamilishaji.

‘Halmashauri
23 zilizoanzishwa mwaka 2014 ziliidhinishiwa jumla ya shilingi
bilioni52.9 katika mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa
majengo ya utawala ya Halmashauri. Hadi Februari, 2019 Halmashauri 23
zimepokea jumla ya shilingi bilioni 23 sawa na asilimia 43.4 kwa ajili
ya kuendeleza ujenzi wa majengo ya utawala ya Halmashauri’’ anasema
Waziri Jafo.

Aidha
Waziri Jafo anasema katika kuzijengea uwezo Tawala za Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa, Serikali katika mwaka 2018/19 imetoa mafunzo kwa
Wakuu wa Wilaya 27 walioteuliwa Oktoba, 2018 katika nyanja za mifumo,
taratibu za mawasiliano Serikalini na mahusiano baina ya Taasisi za
Serikali.

Kwa
mujibu wa Waziri Jafo, mafunzo hayo yameimarisha utendaji kazi wa Wakuu
wa Wilaya katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, utawala bora na
utatuzi wa kero za Wananchi, na pia Mwezi Desemba 2018, Wakuu wa Mikoa
26 na Makatibu Tawala wa Mikoa 26, Wakurugenzi wapya wa Halmashauri 39
walioteuliwa walifanyiwa mafunzo juu ya utawala bora.

‘Vilevile,
Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mipango na Uratibu 26 wa Mikoa na Maafisa
Mipango185 wa Halmashauri walipatiwa mafunzo kuhusu mipango na Bajeti,na
mafunzo hayo yamesaidia kuboresha utendaji ndani ya Serikali na kutatua
kero za wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma’’ alisema Waziri Jafo.

Mamlaka
za Serikali za Mitaa ni vyombo vya wananchi vinavyowawezesha wananchi
kuwa na sauti katika maamuzi mbalimbali ama kwa kushiriki moja kwa moja
au kupitia kwa wawakilishi wao katika shughuli za maendeleo na utawala.