Waandishi wa habari arusha wapongezwa kwa umoja madhubuti

*Viongozi APC wamwagiwa sifa kutetea maslahi ya waandishi bila ubaguzi 

*Dc awasihi kujiunga na chama haraka

Waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda

 Na Seif Mangwangi, Arusha

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda ameupongeza uongozi wa chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Arusha (APC), kwa kuwaunganisha waandishi wa habari Mkoani humo na kutetea maslahi yao bila ubaguzi.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na baadhi ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha, Mtanda amesema tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, ameweza kushuhudia umoja wa kipekee miongoni mwa waandishi tofauti na kwingine.

Amesema ili kuboresha umoja huo waandishi wote wanapaswa kujiunga na chama cha waandishi wa habari mkoani humo kwa kuwa kwa kufanya hivyo wataweza kujadili kwa upana maslahi yao na kuyapatia ufumbuzi kwa haraka.

” Ndugu zangu niwakumbushe tu kuwa umoja wenu ndio silaha madhubuti dhidi ya adui, nawasihi sana waandishi ambao sio wanachama wa APC basi wajiunge na chama, nawapongeza sana viongozi kwa kazi nzuri wanayoifanya,”Alisema.

Amesema tangu amefika Arusha ameweza kushuhudia viongozi wa APC wakiunganisha waandishi wa habari hasa inapotokea waandishi wa habari wanapopatwa na madhila mbalimbali ikiwemo kukamatwa na Polisi.

Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya katika hafla hiyo, Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Seif Mangwangi alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa APC hivi sasa ina wanachama zaidi ya 80 idadi ambayo bado ni ndogo kulingana na idadi ya waandishi wa habari walioko Jijini Arusha.

Amesema miongoni mwa mikakati ya APC ni pamoja na kuongeza idadi kubwa ya wanachama na kutoa wito kwa waandishi wa habari kujiunga na chama kwa kuwa masharti ni rahisi ambayo kila mwenye nia anaweza kujiunga ndani ya saa kadhaa.

” Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya APC tunawakaribisha sana waandishi kujiunga na chama na masharti ni mepesi sana, hata hivyo pamoja na kwamba baadhi sio wanachama bado tumekuwa tukifanya utetezi dhidi yao bila ubaguzi hasa wanapopatwa na madhila au kupoteza wapendwa wao,”amesema.

Mangwangi ametoa wito kwa waandishi wa habari kumsaidia Mkuu wa Wilaya Said Mtanda na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa  kuandika habari nzuri za maendeleo  ya Jiji la Arusha kwa kuwa kwa kufanya hivyo wilaya ya Arusha itang’ara ndani na nje ya nchi.

“Ndugu zangu mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe, nawaombeni sana tumsaidie Mkuu wetu wa Wilaya Said Mtanda kuandika mambo mazuri yaliyopo Arusha, ameteuliwa hapa na Mheshimiwa Rais ili amsaidie kazi na sisi ndio wa kusaidia kuonyesha kazi anazofanya,”Amesema.

Kwa upande wake mwakilishi wa Channel Ten Mkoa wa Arusha,  Jamila Omari amewataka waandishi kujiunga na chama cha waandishi wa habari ili waweze kujumuika na waandishi wengine na kuongeza umoja uliokuwa imara zaidi.

” Waandishi wenzangu mimi ni miongoni mwa waandishi wa habari wakongwe nchini, nimeweza kushuhudia mengi ila suala la kuwa wamoja sio la kufanyia mchezo wala mzaha, nawaomba mjiunge na APC ili kuimarisha umoja wetu kama waandishi, viongozi waliopo wanafanyakazi nzuri sana na mimi nawaunga Mkono,”amesema Jamilla.

Akieleza malengo ya hafla hiyo, mmoja wa waandaaji  mwakilishi wa kituo cha Global TV kanda ya kaskazini, Victor Korumba amesema hafla hiyo ni mwendelezo wa shughuli mbalimbali zinazofanywa kila mwaka kwa lengo la kuwakutanisha waandishi na kufurahi pamoja.

Amesema hafla hiyo inafanyika kwa mara ya pili na Mkuu wa Wilaya  Said Mtanda amealikwa kuwa mgeni rasmi kwa kuwa amekuwa akiweka mbele maslahi ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha na kila mara anapotafutwa amekuwa akitoa ushirikiano wa hali ya juu.

” Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya sisi waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha, pamoja na kwamba miongoni mwetu sio wanachama wa APC lakini tunajivunia kuwa na umoja uliothabiti, na tunakuhakikishia tutajiunga na chama kwaajili ya manufaa yetu sote. Pia tunakuhakikishia tutaendelea kufanyakazi na wewe na hatutakuangusha,” amesema Korumba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *