Waandishi wa habari watakiwa kuhakiki habari zao kabla ya kuchapisha

Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam

Waandishi wa Habari za Mitandao Tanzania wametakiwa kuandika Habari zenye ubora na weledi ikiwa ni pamoja na kutumia Takwimu za uhakika katika kuandaa habari huku wakiacha kuandika vichwa vya habari visivyo na uhalisia ili kuvutia idadi kubwa ya wasomaji ama watazamaji
Rai hiyo imetolewa Novemba 01, 2021 jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Nukta Africa, Nuzulack Dausen katika mafunzo ya Uhakiki wa Habari yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Tanzania (Tanzania Media Foundation TMF).
Dausen amesema kwa sasa Waandishi wengi wa Mitandao wanaandika Habari zisizo na vigezo vya Habari huku wakiacha masuala mengi muhimu ikiwemo takwimu, mizani na ukweli.
Ameongeza kuwa changamoto kubwa inayosababisha hali hiyo ni baadhi ya wamiliki wa Vyombo vya Habari mitandaoni kujali idadi ya watu wanaotembelea mitandao yao bila kuangalia kama habari walizoweka zinasaidia kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Pia Dausen amesema kuwa kwa sasa wasomaji wa mitandaoni wameanza kuzikwepa taarifa zenye vichwa vya habari vya kuvutia ambavyo haviendani na uhalisia wa habari zenyewe.
Awali akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Dastan Kamanzi amesema Waandishi wa Habari wanatakiwa kuwa na msingi wa awali, jumla na wa kubobea katika uandikaji wa habari.
Kamanzi amesema msingi wa uandishi wa Habari ni ukweli hivyo ni muhimu Waandishi wa Habari kuzingatia msingi huo kila wanapoandaa habari zao.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, Joseph Mwaisango pamoja na Asha Shaban wamekiri kwamba yatawasaidia kuboresha uandishi wao wa habari hususani kutumia takwimu na kuhakiki habari kabla ya kuchapishwa mtandaoni.
Mafunzo hayo ya Uhakiki wa Habari yamewajumuisha Waandishi wa Habari za mtandaoni kutoka mikoa ya Shinyanga, Tabora, Mwanza, Arusha, Dodoma, Mara, Mbeya na Iringa.

Mkurugenzi mtendaji wa Nukta Africa Nuzulack Dausen akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya uhakiki wa taarifa kwa waandishi wa habari za mtandaoni yanayofanyika jijini Dar es salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Dastan Kamanzi akifungua mafunzo hayo.
Washiriki wakifuatilia mafunzo hayo.
Picha na Mussa Said, TMF