Neema Mandabila, Mbunge Viti Maalum Songwe |
Na Seif Mangwangi, Arusha
Wabunge Viti Maalum Neema Mandabila kutoka Mkoa wa Songwe na Hawa Mchafu wa Pwani wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake ya kutangaza kutenganisha wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia na watoto.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, wabunge hao wamesema hatua ya Rais inaonyesha ni namna gani amekuwa na mapenzi mema na watanzania na amekuwa na nia ya kuwaletea maendeleo.
Wamesema kwa miaka mingi wao kama wabunge vinara wa masuala ya ustawi wa jamii ( Parliamentary Social welfare focus), na viongozi wa kikundi hicho wamekuwa wakiishauri Serikali kutenganisha wizara hiyo kwa kuwa imekuwa ikishughulikia mambo mengi na mengine kusahaulika.
” Shughuli za Maendeleo ya jamii ni nyingi sana, na muda mrefu zimekuwa zikishindwa kutekelezeka kwa kukosa aidha fedha za kutosha kutekeleza miradi ya maendeleo au pesa nyingi kupelekwa kwenye sekta ya afya,, lakini kwa kitendo hiki tunaamini pesa zitapatikana na bajeti itatosha, “wamesema.
Wamesema kitendo cha Rais kufanyia mabadiliko wizara hiyo, hivi sasa masuala ya maendeleo ya Jamii yatajadiliwa kwa undani na matokeo yake yataonekana wazi tofauti na hapo nyuma.
Neema ambaye ndiye Mwenyekiti wa kundi la wabunge vinara wa ustawi wa jamii ( Parliamentary Social Welfare Focus), amesema kwa kushirikiana na wabunge wenzake atahakikisha matarajio ya Rais Samia Suluhu Hassan mara baada ya kutenganisha wizara hiyo yanatekelezwa na kuifanya wizara ya Maendeleo ya jamii kuwa kiungo muhimu dhidi ya wizara zingine.
“Mambo yote ya uchumi wa mwananchi mmoja mmoja yanajadiliwa kupitia wizara ya maendeleo ya jamii, Saccos,vicoba na hata Tasaf iko wizara hii, kilimo bora kinajadiliwa huku, kwa hiyo hii ni wizara Mtambuka inayotakiwa kupewa kipaumbele kikubwa sana, na mimi kama Mbunge nitamsaidia Rais kutekeleza matarajio yake,”amesema Mwema.
Wabunge Neema Mandabila na Hawa Mchafu |
” Rais Samia ameamua kuwapatia watanzania Maendeleo, sisi kama wasaidizi wake hatutamuangusha, nitoe wito tu kwa Maafisa maendeleo ya jamii kuchapa kazi, tunaamini sasa bajeti yao itapatikana vizuri na hawa maafisa Maendeleo wataenda vijijini kweli kutoa semina za maendeleo,” Amesema Hawa.