Baadhi ya wanawake wa Kijiji cha Tulieni wakiwa wamepumzika baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa tanki la maji unaoendelea kwenye Kijiji hicho cha Tulieni. |
Mhandisi Idd Pazi ambaye ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lindi akipiga hesabu kwenye simu yake ya mkononi alipotembelea mradi wa ujenzi wa tanki la maji linalojengwa Kijiji cha Tulieni.
|
Baadhi ya mafundi wakiendelea na ujenzi wa tanki la maji ambalo ni sehemu ya mradi wa maji Tulieni unaotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19. |
Mkazi wa Kijiji cha Tulieni Zainab Ndembo (katikati) akielezea jambo kuhusu mradi huo wa maji unaotekelezwa kwa fedha za UVIK0-19.
|
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV-Lindi
KATIKA kuhakikisha wanalipa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kupata mradi mkubwa wa maji kupitia fedha za Ustawi maarufu kama fedha za UVIKO-19 wananchi wa kijiji cha Tulieni kata ya Londo, wilayani Lindi mkoani Lindi wamesema katika Uchaguzi Mkuu mwa mwaka 2025 watahakikisha wanamchagua kwa kura nyingi ili aendelee kuwapelekea miradi mingine ya maendeleo.
Wamesema kwa zaidi ya miaka 30 hawahawaji kuwa na maji safi na salama ambayo yanatoka kwenye mabomba lakini chini ya uongozi wa Rais Samia na Serikali yake ya Awamu ya Sita wanaona hilo limetekelezwa kwa kupatiwa mradi wa maji wa Maji Tulieni unaotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 unaogharimu Sh.milioni 421.
Baadhi ya wananchi ambao wamepitiwa na mradi huo, wamewaambia waandishi wa habari wanaotembelea miradi ya maji inayotekelezwa kwa fedha hizo za UVIKO-19 kwamba Serikali kwa kutambua umuhimu wa kupeleka maji kwenye kijiji choa, nao wataonesha umuhimu huo kwa kumpatia kura nyingi Rais Samia pindi uchaguzi mkuu ujao utakapofanyika mwaka 2025.
Wamesisitiza kwamba uamuzi wa Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kuwapatia maji ni wa kuungwa mkono na kupongezwa.
Mkazi wa Kijiji cha Tulieni Zeinab Ndembo pamoja na kuonesha kufurahiswa kwake na kuwepo kwa mradi huo ameelezea namna ambavyo sasa wanakwenda kuondokana na adha ya maji.
”Tumekuwa tukipanda milima na mabonde kwa ajili ya kutafuta maji.Kuja kwa mradi huu kwetu ni faraja na hakika tutaendelea kuwa pamoja na Serikali yetu.”
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa kijiji cha Tulieni Asha Nalika ameeleza walikuwa wanatumia muda mrefu kufuata maji hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha shughuli za maendeleo.
Akizungumza kuhudu utekelezaji wa mradi huo Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lindi Mhandisi Iddi Pazi, amesema ujenzi wa miradi hiyo umefikia asilimia 59 kwa ujumla.
Amefafanua miradi inayotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 miwili wa Kijiji cha Moka Mchinga na Tulieni Mtama inatekelezwa kwa fedha hizo Sh.milioni 800 ambapo mradi wa Tulieni umetengewa Sh.milioni 421 na Moka Sh.milioni 437.Kukamilika kwa mradi huo kwa mujibu qwa Mhandisi Pazi zaidi ya watu 2,000 watanufaika na maji yatatoka katika miradi hiyo miwili.
Mwisho