Wanufaika wa tasaf kusajiliwa kielekroniki, wapigaji sasa basi


Na Mwandishi Wetu, APC KAGERA

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Magata baada ya kumaliza mkutano na wananchi na wanufaika wa TASAF katika Kijiji cha Magata, wilayani Muleba mkoani Kagera. 
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiwa na moja ya familia ya mnufaika wa TASAF katika Kijiji cha Magata wilayani Muleba ambaye alipata ulemavu wa viungo kutokana na ajali

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiangalia banda la mifugo katika Kaya ya mmoja wa wanufaika wa TASAF, Bi. Nazifa Naziru katika Kijiji cha Magata wilayani Muleba.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Mhandisi Richard Ruyango na baadhi ya Watendaji wa TASAF wakielekea kwenye nyumba ya mnufaika wa TASAF kuona namna alivyotumia ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia mfuko huo

Serikali imesema imejipanga kikamilifu kuhakikisha inaweka mkakati madhubuti na endelevu wa kuwapata wanufaika stahiki wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kuwapatia ruzuku zao kwa wakati. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akizungumza na wananchi na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Vijiji vya Magata na Kyamyorwa, wilayani Muleba mkoani Kagera ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Dkt. Mwanjelwa amesema kuanzia sasa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini watasajiliwa katika mfumo wa kielektroniki ikiwa ni pamoja na kupigwa picha kwa anayesajiliwa na anayesajili wakiwa katika makazi ya mnufaika ili kujiridhisha na sifa za mhusika.

Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, katika kuboresha utekelezaji wa Mpango wa TASAF awamu ya tatu sehemu ya pili, wanufaika wa Mpango watapatiwa ruzuku yao kwa njia ya miamala ya simu ili wapate stahiki zao kwa wakati.

“Wanufaika mnatakiwa kuwa na simu za viganjani zitakazowawezesha kupokea ruzuku zenu halisi na kwa wakati,” Dkt. Mwanjelwa amesema.

Dkt. Mwanjelwa amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kuwajali wanyonge hivyo, itahakikisha kila mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini anapata stahiki yake.