Waziri jaffo azindua mfumo wa solar vituo vya mafuta vya orxy

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dk.Seleman Jafo akikata utepe kuashiria kuzindua Solar Energy katika Kituo cha Mafuta cha Oryx Mwenge jijini Dar es Salaam .Wengine katika picha hiyo ni maofisa wa Oryx Energies wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Kalpesh Mehta

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dk.Seleman Jafo akikata utepe kuashiria kuzindua Solar Energy katika Kituo cha Mafuta cha Oryx Mwenge jijini Dar es Salaam .Wengine katika picha hiyo ni maofisa wa Oryx Energies wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Kalpesh Mehta.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Oryx Energies Tanzania Limited Kalpesh Mehta akizungumza na waaandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mfumo wa Solar energy katika Kituo cha Mafuta cha Oryx kilichopo Mwenge jijini Dar es Salaam.Kampuni hiyo imeamua kuja na mkakati wa kutumia Solar energy katika vituo vyake vya mafuta pamoja na maghala yao ya kuhifadhi mafuta nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk.Seleman Jafo akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kampuni ya Oryx Energies Tanzania Limited wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Kalpesh Mehta baada ya kuzinduliwa kwa mfumo wa Solar energy katika kituo cha mafuta cha Oryx Mwenge jijini Dar es Salaam.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dk.Seleman Jafo akikagua kituo cha mafuta cha Oryx kilichopo Mwenge jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais –Mazingira Dk.Seleman Jafo ameipongeza Kampuni ya Oryx  Energies Tanzania Limited kwa hatua inazochukua kwenye kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ametoa pongezi hizo leo Februari 24,2023 jijini Dar es Salaam wakati akizundua mfumo wa matumizi ya Solar energy (Umeme jua) katika kituo cha Mafuta ya Oryx kilichopo Mwenge ikiwa ni sehemu ya kuanza kutumia Solar katika vituo vyao vyote vya mafuta pamoja na maeneo yao ya maghala ya kuhifadhi mafuta nchini.

“Katika kujali mazingira Oryx Energies mmeamua kujielekeza katika matumizi ya Solar ambapo mimi kama Waziri mwenye dhamana na mazingira nawapongeza kwa juhudi kubwa na ya mfano hapa nchini kwetu, hongereni.

“Hii yote inanipa ishara maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuzitaka taasisi za serikali na binafsi  kuhakikisha wanatengeneza mipango inayojali kupambana na mabadiliko ya tabianchi na ninyi Oryx energies mmeamua kujipambanua na kutekeleza maelekezo ya Rais Samia.

“Kwa kweli nawashukuru kwa jambo hili kubwa binafsi najivunia uwepo wa Oryx kwani tangu nilipoingia kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais jukumu langu kubwa ni kuhakikisha tunapambana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ,na kuyafanya mazingira yetu yawe salama .Kama mnavyofahamu sasa hivi dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi ,tunashuhudia barafu zikiyeyuka.

“Ukame uliokithiri katika maeneo mbalimbali , kupungua kima cha maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme na mnakumbuka hivi karibuni nchi yetu ilikumbwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa nishati ya umeme.Hivyo ni wajibu wetu kama  taifa kuungana na mataifa mengine kutumia nishati iliyokuwa salama zaidi ,”amesema.

Waziri Dk.Jafo amesema kuwa katika maendeleo endelevu lengo la saba la malengo ya milenia linasema tutumie nishati za kisasa kwa ajili ya kuzalisha nishati mbalimbali , hivyo Oryx Energies wameamua kulifanya hilo huku akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Energes Kalpesh Mehta kwani ameamua kujipambanua .

Aidha amesema Oryx  Energies imekuwa mfano  wa kuigwa na hiyo imejionesha kwenye maelezo yao kuwa wanazalisha KWh 21  na matumizi yao ni KW tisa , hivyo malengo yao ni kupeleka ziada ya umeme wanayozalisha kwa kutumia Solar energies katika gridi ya Taifa.

“Ametumia fursa hiyo kuziomba kampuni nyingine zote za mafuta kama zitaiga mfano mzuri wa Oryx Energies wa kutumia nishati mbadala sababu watapunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.“Kuja na mfumo wa kutumia umeme wa jua ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kupunguza hewa ukaa ambapo pia huo ndio mkakati za Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia.”

 Kuhusu matumizi ya kuni na mkaa katika kupikia, Waziri Jafo amesema zimesababisha janga kubwa kwani takriban hekari 400,000 kwa mwaka zinapotea kwa ajili ya kuni na mkaa , hivyo matumizi ya gesi yanapoongezeka yanasaidia katika utunzaji wa mazingira.

 “Niwaombe Oryx na kampuni nyingine kama kutakuwa na uwezekano watu wakakopeshwa mitungi na wakawa wanalipa pindi wanaponunua gesi itakuwa ni jambo nzuri la kuwawezesha wananchi wengi kutumia gesi , kwa mfano jiji la Dar es Salaam linaoongoza kwa kutumia mkaa na kuni licha ya kuwa jiji ambalo lina watu wengi waliosoma na wenye kipato.”

Aidha ametoa maelekezo kwa vituo vyote vya mafuta vinavyoanzishwa nchini kuhakikisha wanaweka eneo maalum kwa ajili ya mitambo ya gesi kwenye magari na hiyo itakuwa sifa kuu ya kutoa kibali kwa anayeanzisha kituo cha mafuta.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Energies Tanzania Limited Kalpesh Mehta amesema wanayo furaha kwa kituo cha Mwenge jijini Dar es Salaam kimeanza kutumia nishati ya umeme wa jua(Solar Power) na kwamba hiyo ni hatua ya kwanza kwani watakwenda hatua 10 zaidi kwa nchi nzima kwenye vituo vyao  vya mafuta pamoja na maghala ya kuhifadhi mafuta ambako watatumia ishati ya umeme wa jua.

“Hivyo tumefurahi kuja kwa Waziri Dk.Jafo na amesema mameno mazuri ambayo yametupa nguvu ya kuendelea kufanya vitu vingi na mwaka huu na mwaka ujao tutafanya kazi nyingi na tuhakikisha vituo vyote vinatumia umeme wa jua .Tumeamua kutumia Solar kwani itasaidia kupunguza gharama kubwa, hivyo mikakati yetu ni kutumia umeme jua katika vituo vyetu vyote pamoja na maghala yetu ya kuhifadhia mafuta .”

Aidha amesema Wahandisi wao wamefanya kazi nzuri kwa kuweka mfumo mzuri wa kuhakikisha mfumo wa Solar energy unatumika saa 24 na kuhusu mipango ya Oryx Energies kuweka vituo vya kujaza gesi kwenye magari amesema ni jambo ambalo wanalifanyia kazi kwa kuzungumza na wadau mbalimbali wakiwemo wanaoweza kuweka mifumo ya mabomba ya gesi.

 “Tumeanza kuzungumza na wadau wanaohusika na gesi kwa ajili ya kuweka miundombinu kwa ajili

Akizungumzia upande wa gesi ya kupikia, amesema wameendelea kumahasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia na hivi karibuni walikuwa mkoani Tanga na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ambapo wamegawa bure mitungi 600 kwa wanawake wajasiriamali.