Idris aripoti tena polisi makosa ya mtandao…anatuhumiwa kusambaza uongo na kujifanya rais

Na Pamela Chilongola, Mwananchi 

 Mchekeshaji na mshindi wa shindano la Big Brother 2014, Idris Sultan
ameripoti kituo cha polisi kati leo Ijumaa Novemba Mosi, 2019 na
kuhojiwa kwa dakika 30 na kutakiwa kuripoti tena Jumatano Novemba 6,
2019.
Jana asubuhi, Idris aliripoti kituoni hapo na kuhojiwa kwa saa tano na
kupekuliwa nyumbani kwake, usiku aliachiwa kwa dhamana akitakiwa
kuripoti tena leo saa 2 asubuhi, jambo ambalo amelitekeleza.
“Idris ameripoti kituoni saa 2:00 asubuhi na kuhojiwa kwa dakika 30.
Wamechukua simu zake kwa uchunguzi na kutakiwa kuripoti tena Jumatano
ijayo (Novemba 6, 2019).”
“Wamemueleza kuwa kosa lake ni kusambaza habari za uongo chini ya
kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandao. Kosa la pili ni
kujifanya Rais chini ya kifungu cha 15 cha makosa ya mtandao,” amesema,
Benedict Ishabakaki ambaye ni mwanasheria wa mchekeshaji huyo.
Jana alipopekuliwa nyumbani kwake polisi walichukua kompyuta mpakato kwa
ajili ya uchunguzi, aliporudishwa kituoni kabla ya kupewa dhamana
alipelekwa kitengo cha makosa ya mtandaoni.
Juzi mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alimtaka Idris kuripoti
polisi baada ya kuweka picha yenye sura yake huku akiwa ameketi katika
kiti chenye nembo ya Taifa.
Pia, Idris aliweka picha nyingine inayoonyesha sura ya Rais John
Magufuli akiwa amesimama huku amevaa suruali yenye mikanda inayoshikizwa
mabegani.
Hata hivyo, dakika chache baada ya Makonda kumtaka msanii huyo kuripoti
polisi, waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliahidi
kumuwekea dhamana iwapo angekamatwa.
Ilivyokuwa
Via>>Mwananchi