Akina mbowe na vigogo wengine chadema wafunga ushahidi, hakimu amuonya halima madee na ester bulaya

Shahidi
namba 13 katika kesi ya jinai inayowakabili Mwenyekiti wa CHADEMA,
Freeman Mbowe & wenzake ambaye ni mwanafunzi wa DIT, Lumola Kahumbi
ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa polisi walichukua fedha
zake na kumlazimisha kuimba wimbo wenye maneno Dola si lelemama.


Katika kesi hiyo mawakili wa upande wa utetezi Peter Kibatala, Profesa
Abdallah Safari na upande wa mashtaka wanaongozwa na wakili wa serikali
mkuu, Faraja Nchimbi.

Akiongozwa na Kibatala, shahidi huyo amesema katika kituo cha daladala
cha Kinondoni Studio wakati akielekea kwa shangazi yake, polisi
waliwakamata watu kadhaa na kuwapeleka kituo cha polisi cha Oysterbay.

Amesema akiwa kituoni hapo, waliulizwa kama wanataka kwenda msalani na
wakati anakwenda polisi wawili walimsindikiza na mmoja alimtaka
ajiongeze.

Amebainisha kuwa askari mmoja alimsachi mfukoni na kuchukua Sh12,700
huku akimtaka aondoke bila kugeuka nyuma. Amesema alibaki na Sh200
mfukoni na alilazimika kutembea kwa miguu kutoka kituoni hapo hadi
zilipo hosteli za chuo hicho.

Baada
ya Maelezo ya shahidi huyo, upande wa utetezi katika kesi hiyo ulisema
umefunga ushahidi baada ya kuwaleta mahakamani mashahidi 15 badala ya
200 walioahidi.


Sasa
kinachosubiriwa ni majumuisho ya kesi hiyo yatakayowasilishwa na upande
wa utetezi na ule wa mashtaka Februari 24, 2020 siku ambayo itapangwa
tarehe ya hukumu ya kesi hiyo.

Hakimu
Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba baada ya
kusikiliza maelezo hayo aliwaonya washtakiwa, Halima Mdee (Kawe) na
Ester Bulaya (Bunda)  kwa kukiuka masharti ya dhamana yao baada ya
kutoka nje ya Tanzania bila kibali cha mahakama.

Hakimu
huyo ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 24, 2020 siku ambayo pande
zote mbili zitawasilisha majumuisho yao kabla kupangwa tarehe ya hukumu.